Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUMU: Nyuma ya pazia michezo ya kubahatisha

Muktasari:

Michezo ya kubahatisha maarufu kama ‘kubet’ ndiyo habari ya mjini kwa sasa.


Dar es Salaam. Michezo ya kubahatisha maarufu kama ‘kubet’ ndiyo habari ya mjini kwa sasa.

Ukiacha aina mbalimbali za michezo hiyo zilizokuwepo kwa miaka mingi na katika maeneo maalumu kama vile kasino, hivi karibuni imeibuka ile ya kutabiri michezo na mashine za kutumia sarafu ambayo imesambaa maeneo mengi nchini.

Vilevile, tofauti na miaka ya nyuma, michezo hiyo kwa sasa inachezwa kwenye redio, televisheni, kwenye kompyuta na hata kwenye simu za mkononi.

Nyuma ya pazia ya michezo hiyo, mbali na faida kubwa wapatayo waendeshaji, zipo taarifa mbalimbali tamu na chungu za watu kupata au kuchana mkeka kama wanavyosema vijana, wakimaanisha kupoteza pamoja na wengine kadhaa kupata uraibu.


Faida, hasara zake

“Michezo ya kubahatisha inachangamsha akili lakini pia ukichanga karata zako vizuri unapata fedha. Kwa mfano ukiondoa biashara ya bodaboda, betting inafuata kwa kuwashughulisha watu hususani ni vijana,” alisema Aidan Joseph ambaye ni mshiriki wa michezo hiyo.

Anasema wapo watu ambao kubet kumewatoa (kumewainua) na wengine wanaendelea kupambana, wanapoteza mara kwa mara kwa kuwa michezo ya kubahatisha ina kupata na kukosa.

Hata hivyo, anasema kwa asili michezo ya kubahatisha inapaswa kuwa burudani isiyo na madhara, michezo kama kasino, bahati nasibu, mashine za slots, bingo na aina nyingine inapaswa kuwa kwa ajili ya kujiburudisha si mbadala wa ajira wala chanzo cha kujipatia kipato.

Kulingana na taarifa ambazo Mwananchi limezipata, wapo wanaocheza kwa kuzingatia bajeti waliyoipanga na kwa wakati husika, hivyo kuweka uwiano wa kufanya mambo mengine ikiwamo kupata mahitaji muhimu wao na familia zao, huku wengine wakiwa tofauti.

“Wengine wanacheza hadi kupitiliza, hali ambayo huwasahaulisha majukumu muhimu ikiwamo kujipatia mahitaji muhimu na kuhudumia familia zao,” alisema moja wa wachezaji.

Mshiriki huyo aliyejitaja kwa jina moja la Shilton wa Dar es Salaam, alisema alianza kujihusisha na michezo hiyo miaka minne iliyopita na kilichomfanya kuwa muathirika ni namna alivyokuwa akishinda pesa.

“Nakumbuka niliweka elfu hamsini kwa kuzichagua Manchester United, PSG, Barcelona na Ajax na nilibashiri vipindi ambavyo vitatoa mabao mengi. Ilikuwa kama utani vile mambo yakajipa nikapiga laki tano kwa mara ya kwanza, nikaanza kuona kumbe hii inaweza kuwa kazi badala ya kuendelea na ujasiriamali. Niliacha ujasiriamali nikamwachia mke wangu,” alisema

Shilton anasema alikuwa anatumia muda mwingi kuchambua mechi na kubeti, mwisho akajikuta akikosa pesa, akafikia kuuza vitu vyake vya ndani. Aliuza televisheni na kitanda baada ya kumdanganya mkewe kuwa mama yake alikuwa mgonjwa, hivyo zilihitajika pesa za matibabu.

“Wakati hayo yanatokea, si kwamba kila siku unakosa, kuna wakati unapata. Pesa kubwa ambazo nimepata kwenye kubeti siwezi kusahau, ni Sh10 milioni ambazo zilinisaidia kumalizia ujenzi wa nyumba yangu,” alisema.

Jimmy Charles, mkazi wa Arusha alisema kuna siku alikuwa na Sh1 milioni moja mkononi ambazo aliona angeweza kuzizalisha maradufu au zaidi kupitia kubet.

“Niliingia hotelini kucheza (kamali) kuanzia asubuhi, nilianza kwa kushinda nikafikisha Sh3 milioni, nikaona bado naweza kupata pesa zaidi, lakini kibao kiligeuka. Ile nastuka saa tano usiku na sina hata senti kumi mfukoni. Wakati huo niko maeneo ya Philips na nyumbani ni Njia Panda ya Mbauda, nilipagawa na siwezi kuisahau hiyo siku,” alisema.

Hata hivyo, alisema michezo ya kubahatisha ina faida, ila la msingi ni kuwa na nidhamu na hasa kucheza kwa kiasi.

Mmoja wa watoa huduma za michezo hiyo eneo la Kinondoni, Dar es Salaam (hakutaka kutajwa) alisema faida inayopatikana kwenye michezo hiyo ni kubwa, mfano kituo alichopo wamekuwa wakiingiza zaidi ya Sh300 milioni hadi 500 kwa wiki. “Ni kweli kuna vijana ambao wamegeuza mchezo huu kama sehemu ya ajira yao ya kujiingizia kipato, hawa wanahitaji kutambua kuwa hii ni bahati nasibu, wajenge tabia ya kucheza kwa kiasi, ukipata basi, nenda nyumbani au katumie fedha hizo kufanya mambo mengine.


Uraibu

Kutokana na kucheza mara kwa mara baadhi ya watu hupata uraibu wa michezo hiyo.

Huenda matatizo haya Tanzania hayajaonekana sana ila yapo kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika michezo hiyo.

“Huyo jamaa uliyepishana naye kila siku yuko hapa isipokuwa wakati ule Uviko-19 hakuonekana sana, akianza kucheza habanduki, chai inamkuta hapa, chakula cha mchana hapa hadi usiku tunapofunga,” alisema Pancras Oscar akimwelezea mteja wake mmoja katika moja ya vituo vya michezo ya kubahatisha (betting).

Akizungumza na gazeti hili Oscar ambaye anasimamia kituo hicho kilichopo Magomeni jijini Dar es Salaam, alisema wapo wengi wanaotumia muda mwingi katika eneo hilo ila idadi imepungua miaka ya karibuni kwa sababu ya kukua kwa teknolojia, kwa kuwa wengi wanacheza kupitia simu za mkononi.

Grace Njiku ambaye anafanya kazi katika moja ya kasino jijini Dar es Salaam anasema kuna wateja ambao mara kwa mara wanakuwa katika michezo hiyo ambao humaliza hadi siku tatu bila kutoka nje.

“Ujue kasino kila kitu kinapatikana ndani, kwa hiyo kama hela unayo unaweza kukaa humohumo, kuna watu wanacheza wanaliwa hadi tunawakopesha ili waendelee kucheza,” alisema Njiku.


Kauli ya wasimamizi

Taarifa za Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT) zinaonyesha watu wanaokumbwa na uraibu wa michezo ya kubahatisha nchini si zaidi ya 10 kwa mwaka, wengi wao ni vijana wanaocheza michezo hiyo kwenye Kasino.

“Mwaka 2020 idadi ya watu tuliowatambua kwa uraibu na kuwasaidia walikuwa 10, mwaka 2021 walikuwa saba, wote ni wanaume na vijana, hasa wale wanaobahatisha kwenye michezo (sports betting), hususani za mitandaoni

Uraibu ni hatua inayomgharimu muhusika kwa sababu bila kucheza anaweza hata akaumwa,” anasema James Mbalwe, mkurugenzi mkuu GBT.

Mbalwe alisema GBT ina jukumu la kulinda jamii dhidi ya matokeo hasi yanayoweza kutokea kwa kushiriki michezo ya kubahatisha.

Alisema GBT ipo makini katika kusimamia michezo ya kubahatisha kwa kuwa ni eneo ambalo ni muhimu kiuchumi lakini lisiposimamiwa vizuri linaweza kuleta madhara kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Kwa sasa tunauunda mfumo wa kutusaidia kufuatilia wachezaji wote wa michezo hiyo hapa nchini na kuchunguza viashiria vya uraibu ili kuwadhibiti mapema pindi hali hiyo inapoanza lakini kwa sasa kila mwendeshaji anafuatilia mteja wake na kutupatia taarifa ili kuwapatia matibabu ya kisaikolojia,” alisema.

Alisema pindi mwendeshaji anapomtambua mteja wake kwa viashiria vya uraibu au mteja mwenyewe au familia yake ikiripoti GBT, mhusika huzuiliwa kuingia katika maeneo ya michezo hiyo hata kucheza, hata hivyo aliyezuiliwa anaweza kuomba kurejeshwa endapo atakuwa amebadili tabia zilizoonwa awali.


Mwenye uraibu

Kwa mujibu GBT na kampuni zanazochezesha michezo ya kubahatisha mtu anaweza kujua kuwa amepata uraibu pindi anapocheza michezo ya kubahatisha ili kugharamia mahitaji mbalimbali.

Njia nyingine ya kumtambua au kujitambua ni pale mawazo ya mtu yanapotawaliwa na kucheza kila siku, kuwa msiri juu ya kucheza kwake ili walio karibu naye kama vile marafiki au ndugu wasijue.

Pia mhusika anaanza kujisikia mwenye kosa baada ya kucheza, kuacha kulipa ankara muhimu, kucheza ili kuokoa fedha alizopoteza, kucheza mpaka kuishiwa, kushindwa kupunguza au kuacha kucheza, kushindwa kuhudumia familia kwa sababu ya kucheza na kuathiri utendaji wake wa kazi kwa kushiriki mchezo mara kwa mara.

Kadhalika ishara nyingine ya uraibu ni mtu kuvutana na wanaosimamia juu ya kiwango cha fedha anachocheza, kucheza kwa muda mrefu kuliko uliojipangia, kucheza zaidi ya uwezo wako wa kifedha, kucheza zaidi kipindi unaposhinda au kuliwa na kuambiwa na watu wako wa karibu kuwa umekuwa mraibu na kutamani kujipa adhabu kutokana na kupoteza fedha zako katika mchezo.


Ulinzi wa watoto

Mbalwe alisema kwa mujibu wa vifungu namba 47 na 70 vya sheria ya michezo ya kubahatisha ni kosa kwa mtu yeyote aliyejuu ya miaka 18 kuruhusu au kusababisha mtoto wa chini ya umri huo kushiriki kwenye michezo ya kubahatisha.

Alisema mwendeshaji wa michezo ya kubahatisha anapaswa kuhakiki umri wa wachezaji kabla ya kuwaruhusu kucheza ili kuhakikisha kuwa watu wenye umri chini ya miaka 18 hawaingii.

“Bodi inatoa msisitizo kwa wazazi na walezi kufuatilia mwenendo wa watoto wao ikiwemo mahudhurio shuleni na matumizi yake ya fedha, sanjari na kutomuwezesha mtoto kushiriki katika michezo ya kubahatisha kwa kumpatia vifaa kama simu na kompyuta,” alisema Mbalwe.

Alisema jukumu la kumlinda mtoto dhidi ya michezo ya kubahatisha ni la kila mwananchi hususani mwendeshaji, mwalimu, mzazi, mlezi na pindi mtu anaposhudia kupuuzwa kwa ulinzi huo, anapaswa kutoa taarifa kwenye Bodi ya Michezo ya Kubahatisha au kituo cha polisi.


Shida kisaikolojia

Kutokana na tatizo hilo la uraibu, wanasaikolojia wameonya kuwa michezo ya kubashiri humuathiri mhusika kwa namna nyingi ikiwemo ubongo wake kutaka mafanikio ya haraka.

Mwanasaikolojia Charles Nduku alisema michezo hiyo ililetwa na wazungu na historia inaonyesha kwamba ni ya matajiri, lakini ililetwa nchi za Asia na Afrika na zingine zinazoendelea kwa kuwa walijua vijana wengi hawana kazi, hivyo itakuwa rahisi kwa wao kuishiriki kwa kipato walichokuwa wanapata.

“Wameona watu hawana kazi na hela hawana, hivyo wanazileta kwa kuwa wanaamini watu watabet kwa sababu hawataki kufikiri, ile wanaifanya kama sehemu ya wao kujipatia fedha,” alisema.

Nduku alisema mchezo huo wa kubashiri una uraibu kama ambavyo mtu anakuwa tegemezi kwenye pombe na hapa anakuwa tegemezi wa mchezo huu. Mtu akiingia kwenye hii kitu inahitaji kidogo msaada kumtoa kwenye hii hali.” Anasema mara nyingi mraibu anakuwa na kawaida ya kupenda ugomvi kwani namna anavyofikiri anatarajia matokeo mapema. “Wengi huanza kuhitaji mambo harakaharaka, hawezi kusubiri kwa muda mrefu kwa hiyo betting haimuathiri tu mtu kifedha na kiuchumi lakini inamuathiri namna anavyofikiria na namna ubongo wake anauweka, hata kama akija kuacha ataendelea kutaka mafanikio ya haraka,” alisema Nduku.


Mapata ya Serikali

Licha ya madhara yake, michezo hiyo inatajwa kuwa na faida kubwa kwa waendeshaji na huingiza fedha nyingi kwa Serikali.

Kwa mujibu wa GBT mwaka wa fedha 2020/2021 mzunguko wa fedha katika sekta ndogo ya michezo ya kubahatisha ulikuwa ni miamala yenye thamani ya Sh3.17 trilioni na makusanyo ya Serikali yalikuwa Sh132 bilioni.