Riba kubwa inavyokwamisha wazabuni wa ndani
Muktasari:
- Kafulila amesema tofauti ya riba kati ya kampuni za ndani na nje huathiri ushindani, akihimiza ushirikiano wa umma na binafsi.
Mbeya. Kampuni za ndani zinaendelea kupoteza zabuni kubwa kwa wawekezaji wa kigeni, hususan kampuni kutoka China, kutokana na gharama kubwa za mikopo, imeelezwa.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki katika mhadhara uliofanyika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Mbeya (MCC), ambapo tofauti ya gharama za mtaji ilijadiliwa kwa kina.
Mhadhara huo uliokuwa na kaulimbiu, ‘Nafasi ya vyuo vikuu, sekta ya viwanda na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050’, uliwakutanisha wanafunzi, wahadhiri na wadau wa sekta binafsi kujadili mwelekeo wa Tanzania kuelekea Dira ya 2050.
Akiwasilisha mada kuu kuhusu mageuzi ya uchumi yanayohitajika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, alisema ushindani katika zabuni za umma bado hauko sawa kwa wazabuni wote.
“Tatizo kubwa ni gharama ya mtaji. Kampuni ya China hupata mkopo nchini kwao kwa riba ya asilimia moja, wakati kampuni ya Tanzania hulazimika kukopa kwa riba ya asilimia 18 kutoka benki za ndani.
“Ikiwa kampuni ya China itawasilisha zabuni ya Sh10 bilioni na kampuni ya Tanzania ikawasilisha ya Sh14 bilioni, Serikali haina budi kuchagua zabuni yenye gharama ndogo ili kulinda fedha za walipa kodi,” alisema Kafulila mbele ya ukumbi uliojaa wanafunzi na wahadhiri.
Alisisitiza kuwa, pamoja na umuhimu wa kuimarisha sekta binafsi ya ndani kupitia ushirikiano, Tanzania haiwezi kuzuia uwekezaji wa kigeni, akibainisha kuwa hata Dubai ilijengwa kwa kutegemea asilimia 80 ya uwekezaji kutoka nje.
Alisema tofauti hiyo ya ushindani katika zabuni ni miongoni mwa changamoto ambazo Tanzania inapaswa kuzitatua ili kufikia lengo la kuwa uchumi wenye thamani ya Dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050.
Kafulila alisema kufikia lengo hilo kunahitaji hatua kubwa kutoka katika pato la sasa la taifa (GDP), linalokadiriwa kuwa Dola bilioni 94 za Marekani.
“Ili kufikia uchumi wa Dola trilioni moja mwaka 2050, thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa Tanzania kila mwaka lazima ifikie Dola trilioni moja,” alisema.
“Tunataka uzalishaji wa mwaka 2050 uwe karibu sawa na uzalishaji tulioufikia katika kipindi chote cha miaka 25 iliyopita,” aliongeza.
Alisema safari hiyo itahitaji uwekezaji wa jumla wa Dola trilioni 3.7 za Marekani, akieleza kuwa mapato ya kodi na mikopo pekee hayawezi kugharamia mahitaji hayo, hivyo ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) hauwezi kuepukika.
Alitaja Bandari ya Dar es Salaam kuwa mfano wa mafanikio, akisema kiwango cha mizigo kimeongezeka mara tatu baada ya waendeshaji binafsi kushirikishwa.
“Huku si kuuza nchi, bali ni kuleta utaalamu na mifumo inayofanya kazi,” alisisitiza.
Mbali na changamoto za kifedha, Kafulila alisema Tanzania pia inakabiliwa na upungufu mkubwa wa rasilimali watu, akinukuu takwimu za Benki ya Dunia zinazoonyesha kuwa Kielezo cha Mtaji wa Watu (Human Capital Index) cha Tanzania ni asilimia 40, ikimaanisha mtoto anayezaliwa leo atafikia asilimia 40 tu ya uwezo wake wa uzalishaji.
“Siku hizi mataifa hayashindani kwa idadi ya milima, madini au misitu waliyonayo. Yanashindana kwa ubora wa watu wake,” alisema Kafulila, akisisitiza kuwa watu wasio na ubora wanaweza kuugeuza msitu kuwa jangwa, lakini watu wenye ubora wanaweza kuligeuza jangwa kuwa msitu.
Akizungumzia nafasi ya kijiografia ya Tanzania, alisema ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1,400 katika Bahari ya Hindi unaifanya Tanzania kuwa katikati ya asilimia 90 ya biashara ya dunia inayofanyika kwa njia ya bahari.
Hata hivyo, alionya kuwa faida hiyo ya kijiografia itaendelea kubaki bila manufaa endapo hakutakuwa na maboresho makubwa katika bandari pamoja na mifumo ya usafirishaji na ugavi.
Akizungumzia changamoto za miundombinu ya vyuo vikuu, Kafulila alipendekeza matumizi ya mfano wa “Hoteli ya Rotana.”
Alivitaka vyuo vikuu kuwakaribisha wawekezaji binafsi kujenga mabweni katika maeneo ya vyuo, akisema, “Ukisubiri bajeti ya Serikali, unaweza kusubiri kwa miaka saba. Kupitia PPP, unapata jengo sasa.”
Pia, alisisitiza umuhimu wa ufanisi wa taasisi, akisema unachangia asilimia 25 ya utajiri wa taifa.
Alitoa wito wa kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya kimtazamo ili kuhakikisha Tanzania haifikii asilimia 50 au 60 pekee ya malengo ya Dira ya 2050.
Alichokisema Mkuu wa Chuo
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Mbeya (MCC), Prof Henry Mollel, alisema chuo chake kitaanzisha programu za Stashahada na Shahada ya Kwanza katika masomo ya PPP ili kuongeza wataalamu katika sekta hiyo.
“Utafiti wetu unapaswa kusaidia sekta binafsi kuendesha mifumo ya biashara inayokidhi mahitaji halisi ya nchi,” alisema Prof Mollel.
Mshauri wa Biashara na Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Enok Nyange, alisema nguvu kazi ya baadaye italazimika kukumbatia matumizi ya Akili Unde (AI) na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
“Lazima ujifunze kudhibiti hisia zako na za wengine. Ninaona wahitimu wengi wakipoteza mwelekeo kutokana na msongo wa mawazo,” alisema.
Mhadhiri wa masuala ya fedha chuoni hapo, Dk Adrian Barongo, alisema ingawa asilimia 60 ya mtandao wa barabara sasa umewekwa lami, zama hizi zinatawaliwa na huduma pamoja na teknolojia.
“Ubunifu ni rasilimali isiyoonekana. Msisome kwa ajili ya kufaulu mtihani pekee, fikirieni nje ya mazoea,” alisisitiza.
Hata hivyo, kiongozi wa wanafunzi, Teresia Wunja, alisema utafiti uliofanywa chuoni hapo umeonesha kuwa asilimia 49.7 ya wanafunzi hawaifahamu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kama sisi wasomi hatuijui dira hiyo, vijana walioko mitaani wataijuaje?” alihoji, akipendekeza wasanii maarufu watumike kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kuhusu Dira ya 2050.