RC Songwe awaonya wanaozusha taharuki ya kuibiwa nyeti
Mkuu wa mkoa wa Songwe Jabir Omary Makame akizungumza na wananchi wa Kisimani katika halmashauri ya mji wa Tunduma. Picha na Denis Sinkonde
Muktasari:
- Watu wanne wafariki, 29 wakamatwa kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi.
Tunduma. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, ameonya watu wanaozusha taharuki kwa madai ya kuibiwa nyeti kwa njia za kishirikina, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vinavyohatarisha usalama wa wananchi.
Makame alitoa onyo hilo leo Aprili 3, 2026, wakati wa ziara maalumu aliyofanya katika maeneo ya Kilimanjaro na Kisimani mjini Tunduma, Wilaya ya Momba, kwa lengo la kutuliza hofu iliyozuka miongoni mwa wananchi kufuatia madai ya baadhi ya wanaume kuibiwa au kusinyaa kwa sehemu zao za siri.
Akizungumza na wananchi, Makame amesema Serikali imepokea taarifa za kuongezeka kwa taharuki hiyo ambayo imechochea baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, hali iliyosababisha vifo na majeruhi.
“Hatuwezi kukubali wananchi waishi kwa hofu katika eneo muhimu la kibiashara kama Tunduma. Serikali haitavumilia mtu yeyote atakayezua taharuki au kuchochea vurugu kwa madai ya kupoteza nyeti,” amesema Makame.
Amesema vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyochochewa na imani za kishirikina vinahatarisha maisha ya watu na kuharibu taswira ya Mkoa wa Songwe, ambao ni lango muhimu la biashara mpakani.
“Hali hii inachafua taswira ya mkoa wetu. Mtu yeyote atakayezua taharuki au kuhusika na vitendo hivi atachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesisitiza.
Makame pia amewataka viongozi wa serikali za mitaa kushirikiana na vyombo vya dola katika kudhibiti hali hiyo, huku akieleza kuwa operesheni inaendelea kuwabaini watu wote wanaohusika na matukio ya uchochezi na vurugu.
“Wanaume wenzangu, nawahakikishia endeleeni kufanya kazi zenu bila hofu. Serikali ipo na itahakikisha usalama wa kila mwananchi,” amesema Makame.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema hadi sasa watu wanne wamepoteza maisha na wengine wanne wanapatiwa matibabu hospitalini baada ya kushambuliwa na wananchi waliodai wanahusika na vitendo hivyo.
Amesema pia watu 29 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kufuatia matukio hayo.
Senga ametolea mfano tukio lililotokea Aprili 2, 2026, katika mji wa Vwawa, wilayani Mbozi, ambapo dereva wa bajaji alijeruhiwa na kulazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na wananchi waliodai amehusika na wizi wa nyeti.
Hata hivyo, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo kilikuwa mgogoro wa madai ya fedha kati ya dereva huyo na mtu mwingine, lakini baadaye tukio hilo likageuzwa na kuhusishwa na madai ya kishirikina na kusababisha vurugu.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha kueneza uvumi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapokuwa na mashaka ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.