RC Serukamba ahimiza uwekezaji kwenye kilimo cha miti

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amewahimiza wakulima kuwekeza kwenye kilimo cha miti ambacho mbali na kuinua uchumi wa mkoa huo, kinasaidia kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi
Iringa. Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amewataka wakulima kuwekeza kwenye kilimo cha miti.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya Kampuni ya One Acre Fund Tanzania kutoa motisha ya malipo ya fedha kwa wakulima wa miti, Serukamba amesema licha ya kuwa mkoa huo unajivunia uwepo wa miti, bado inahitajika kasi kubwa ya kupanda misitu mingi zaidi.
“Motisha hii kwa wakulima itawasaidia kuongeza kipato cha ziada ambacho kitawawezesha katika shughuli zao za kilimo na masuala mengine ya kifamilia, hivyo iongeze kasi zaidi kwenye upandaji wa miti tuweze kutunza mazingira,” amesema Serukamba.
Awali, Ofisa Jaribio la Motisha wa One Acre Fund katika Kijiji cha Utengule Wilayani Kilolo, Christina Mgata amesema lengo la mradi huo ni kutoa motisha kwa wakulima ili waweze kutunza miti inayopandwa.
"Mkulima anapewa motisha na kampuni kwa ajili ya kumtia moyo mkulima ili aweze kutunza miti, mradi huu ni mradi wa malipo ya kaboni kwa mkulima ili apande miti na upo kwa ajili ya kulinda mazingira,"amesema Christina.
Ofisa Habari wa kampuni hiyo, Dorcus Tinga amesema mpaka sasa wamesambaza na kupanda miti milioni 2.6 kwa wakulima wote ambao wanawahudumia.
Baadhi ya wakulima walio nufaika na motisha hizo, Dismas Mbigili na Suzana Kaovela wamesema walianza kupata miti kwa kasi baada ya kushawishiwa.
“Mabadiliko ya tabianchi yameathiri mpaka kilimo, misitu tunayopanda itakuwa tiba. Binafsi nimeshawishiwa kupanda miti kwa kasi kubwa na kuitunza,” amesema Mbigili.