Rais wa Chama cha Walimu Tanzania atema cheche

Rais wa Chama Cha walimu Tanzania (CWT) Leah Ulaya akiwa na baadhi ya wanachama wakiimba wimbo wa chama hicho walipokutana kwenye Makao Makuu ya CWT jijini Dodoma
Muktasari:
- Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Leah Ulaya amesema, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri nchini amemuandikia Katibu Mkuu wa Chama hicho barua ya kubatilisha maamuzi ya kikao kilichofanywa na wajumbe 18 wa Kamati ya Utendaji Taifa walioazimia ‘kumsimamisha’ kazi Katibu Mkuu, Japhet Maganga.
Dodoma. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Leah Ulaya amesema, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri nchini amemuandikia Katibu Mkuu wa Chama hicho barua ya kubatilisha maamuzi ya kikao kilichofanywa na wajumbe 18 wa Kamati ya Utendaji Taifa walioazimia ‘kumsimamisha’ kazi Katibu Mkuu, Japhet Maganga.
Leah ameyasema hayo leo Juni 10, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa kikao kilichofanyika Juni 6, 2023 cha wajumbe 18 kati ya 32 wa Kamati ya Utendaji Taifa.
“Ili kuondoa sintofahamu ya kikao hicho batili pamoja na maazimio yake, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania, kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba DA27/380/12/21 ya tarehe 9 Juni, 2023 kwa Katibu Mkuu wa CWT; amebatilisha maazimio ya kikao hicho na utekelezaji wake,” alisema Leah.
Aidha amesema barua hiyo imeeleza kikao hicho kilichoendeshwa chini ya uenyekiti wa Mwalimu Thobias Sanga, hakikuwa halali na kilifanya maamuzi batili ambayo hayakuzingatia Katiba na Kanuni ya CWT.
Aidha Leah amesema kitendo cha wajumbe hao kuitisha kikao hicho alichokiita batili, ni kupoka mamlaka na madaraka ya Rais wa CWT na Katibu wake kinyume, kitu ambacho ni katiba ya chama hicho.
“Kikao hicho kilichofanyika na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa chini ya uenyekiti wa Mwalimu Sanga na Katibu wake ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, ni kinyume na ibara ya 21.3(c) ya Katiba ya Chama, toleo la sita la mwaka 2014.
Pamoja na kanuni ya 5b ya Kanuni za CWT toleo la nne la mwaka 2015 ambapo Rais wa chama ambaye ni Mwenyekiti na Katibu ambaye ndio Katibu wa vikao vyote vya chama ngazi ya Taifa ndio wenye uhalali wa kuitisha vikao vyote vya kitaifa.
Juni 6, 2023 wajumbe 18 kati ya 32 wa Kamati ya Utendaji ya Taifa wa CWT, walikutana kwenye kikao cha dharura katika ofisi za chama hicho Dodoma, kwa lengo la kumjadili Katibu Mkuu, Japhet Maganga wakimtuhumu kutoishirikisha vikao vya kamati kwenye masuala ya fedha, kuwaajiri, kuwahamisha na kufukuza wafanyakazi wa CWT bila kushirikiana na kamati hiyo.