Rais Samia afafanua umuhimu wa SGR

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ana matumaini reli ya kisasa itasaidia kushusha gharama na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa baina ya bandari na sehemu za ndani na nje ya nchi.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akifungua jiwe la msingi la ujenzi wa reli wa kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka ambayo itakuwa na urefu wa kilometa 341.
“Moja ya mambo yanayotajwa kukwamisha kasi ya maendeleo Afrika ni kutokuwepo kwa miundombinu imara ya usafiri, tafiti zinaonyesha kuwa ukosefu na ubovu wa miundombinu sio tu unachelewesha usafirishaji wa watu na bidhaa bali unaongeza gharama za bidhaa kwa asilimia 40,” amesema
Rais Samia ambaye yupo mkoani Mwanza kwenye ziara ya siku tatu amesema mradi huo unatekelezwa kwa vipande na Mwanza wapo kwenye kipande cha tano huku wakiruka kipande cha tatu na nne na tayari vishaanza kufanyiwa kazi.
Ameongeza kuwa shehena ya kwanza ya vichwa vya treni kwa ajili ya majaribia vitafika Desemba mwaka huu na inayofwata itakuja katikati au mwisho wa mwaka 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa hiyo kutoka Mwanza kwenda Isaka utazalisha ajira zaidi ya 86,000 kwa watanzania.
Kadogosa amesema ajira 11,000 zitakuwa za kudumu na ajira zisizo za kudumu zaidi ya 75,000.

Kwa mujibu wa Kadogosa, reli hiyo inayotoka Mwanza hadi Isaka itakuwa na urefu wa kilometa 341.
"Ujenzi huu utagharimu Sh3.1617 trilioni na tayari tumeshajenga kambi kwa ajili ya kuanza ujenzi huu," amesema Kadogosa.
Pia amesema ujenzi wa reli hiyo utasaidia kupunguza gharama na usumbufu kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kulazimika kusafiri hadi mkoani Dar es Salaam kupokea mizigo yao.
Ameongeza kwamba; "Tunataka kuileta Dar es Salaam ije Mwanza badala ya watu kusafiri kwenda kuchukulia mizigo yao Dar watachukulia hapa," amesema Kadogosa.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba usanifu wa reli hiyo umezingatia viwango kiasi cha kuifanya idumu kwa miaka 100.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei, Michael Zhang alisema kwa sasa kampuni hiyo inashirikiana na TRC kutoa vifaa vya mawasiliano na huduma kwenye mradi wa SGR ikiwemo Mfumo Teknolojia ya Mawasiliano-Reli (GSM-R), ambayo baadae itabadilika kuwa mfumo wa LTE- R.
"Niimani yetu kwamba chini ya uongozi mpya wa Rais Samia Suluhu , Huawei itaendelea kujenga miundombinu ya tehama kulingana na dira ya maendeleo ya Tanzania 2025," alisema