Raila Amolo Odinga na ahadi 10 kwa Wakenya-1

Muktasari:
Raila Amolo Odinga, anayefahamika pia kwa wafuasi wake kama Agwambo, Tinga, Baba, RAO na Jakom ni mwanasiasa mkongwe nchini Kenya.
Raila Amolo Odinga, anayefahamika pia kwa wafuasi wake kama Agwambo, Tinga, Baba, RAO na Jakom ni mwanasiasa mkongwe nchini Kenya.
Odinga alijitupa katika ulingo wa siasa nchini Kenya mwaka 1992, alipochaguliwa kuwa mbunge wa Lang’ata.
Aliteuliwa kuwa waziri wa nishati kuanzia 2001 hadi 2002 kisha waziri wa barabara, ujenzi na nyumba kuanzia 2003 hadi 2005.
Alikuwa mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa 2007.
Kufuatia chaguzi zilizofuatia uchaguzi huo, Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika makubaliano ya kugawana madaraka na Rais Mwai Kibaki, Aprili 2008.
Alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa 2013.
Odinga ndiyo kiongozi mkuu wa muungano wa CORD, uliyoundwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013 na ndicho chama kikuu cha upinzani nchini Kenya.
Raila Odinga anaonekana kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake, Jaramogi Odinga.
Alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya baada ya uhuru, lakini aliondoka serikalini mwaka wa 1966 baada ya kutofautiana na kiongozi wa wakati huo, Jomo Kenyatta, baba yake rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.
Jaramogi Odinga aliunga mkono ushirika na uhusiano wa karibu na nchi za Umoja wa Kisovieti na China, huku Jomo Kenyatta akiunga mkono ushirika wa Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yenye nguvu.
Tofauti zao zilizidi kuwa mbaya, ambapo Jaramogi Odinga alifungwa kwa miezi 18 hadi alipoachiwa huru mnamo mwaka 1971.
Raila Odinga pia ni mfungwa wa zamani wa kisiasa, na anashikilia rekodi ya kuwa mfungwa wa kisiasa aliyetumikia kifungo cha muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Mapambano yake dhidi ya udikteta wa chama kimoja yalimfanya awekwe kizuizini mara mbili (kutoka 1982 hadi 1988 na 1989 hadi 1991) wakati wa utawala wa mrithi wa Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi.
Hapo awali alifungwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka wa 1982.
Mpinzani wake wa karibu ni William Ruto wa Chama cha United Democratic Alliance (Uda), Naibu wa sasa wa Rais anayejinadi kwa misingi ya kutetea maslahi ya wananchi wa tabaka la chini waliobandikwa jina ‘Hustler’.
Ahadi za Raila Odinga
Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga, ameahidi Wakenya maisha mema ambayo kila Mkenya atafurahia katika utawala wake endapo atashinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Odinga, ambaye ni mwanawe Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga, anagombea urais katika jaribio lake la tano baada ya kufanya hivyo mwaka 1997, 2007, 2013 na 2017 bila mafanikio.
Anagombea urais mwaka huu kupitia muungano wa vyama vingi vya kisiasa, uliopewa jina Azimio la Umoja.
Shabaha kuu katika manifesto (ilani) ya Raila Odinga ni kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuleta mabadiliko ya kijamii na utawala bora.
Anaahidi Wakenya kwamba ataangazia zaidi namna ya kupunguza gharama ya maisha, kuimarisha huduma ya afya, kubuni nafasi za kazi kwa kila Mkenya, kuhakikisha kila boma lina maji safi, kupambana na ufisadi pamoja na kupambana na uhaba wa chakula.
Odinga, mwenye umri wa miaka 77, analenga kubuni sera zitakazohakikisha gharama za maisha zinashuka maradufu, katika muda wa siku 100 baada ya kuingia madarakani.
Gharama za maisha, elimu bila malipo hadi chuo kikuu
Kulingana na manifesto ya Raila Odinga, ambayo anafanya kampeni kwa kutumia maneno ‘inawezekana’, atapunguza gharama za maisha ndani ya siku 100 kwa kupunguza bei ya mafuta ya petroli, unga, intaneti na nishati.
Walimu wote ambao wamehitimu na hawajapata kazi wataajiriwa punde tu atakapoingia madarakani ili kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ni ya kiwango cha juu.
Zaidi ya hilo, amewaahidi Wakenya kuwa Serikali yake itatoa elimu ya bure kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu.
Kwa kuzingatia kwamba utalii ni mojawapo ya sekta muhimu kwa uchumi wa Kenya, Serikali ya Odinga itawafunga maisha gerezani wawindaji haramu na watu wanaofanya biashara ya pembe za ndovu na vitu vyote vinavyotokana na uwindaji haramu.
“Tutaanza kwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa katika mbuga za wanyama za kitaifa ili kuwanasa wawindaji haramu.
Tutawekeza zaidi katika utafiti namna ya kulinda mali zetu asili.” Amesema Odinga wakati wa uzinduzi wa manifesto yake hivi karibuni jijini Nairobi.
Wanajeshi kuongezewa mshahara
Manifesto ya Odinga inawaahidi wanajeshi wote wa Kenya nyongeza ya mshahara na kuboresha mazingira yao ya kazi, katika muda wa siku 100 baada ya kuapishwa.
Mabadiliko yatafanyika katika idara ya polisi, ikiwemo kuwawezesha polisi kutumia mfumo wa kisasa wa kupambana na uhalifu na kuboresha zaidi kazi yao.
“Tutaweka polisi maalumu sita kwa kila kituo cha polisi ili kushughulikia masuala ya vijana.
“Hili litaboresha uhusiano kati ya polisi na vijana. Tutaboresha mazingira ya kazi ya maofisa wa jeshi,” alijinasibu Odinga.
Itaendelea kesho