Polisi, wananchi washirikiana kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi
Baadhi ya wananchi wa Melela wakiwa katika mkutano na viongozi wa Jeshi la Polisi. Picha na Juma Mtand\a
Muktasari:
- Viongozi wa vijiji na wananchi wanapaswa kushirikiana kwa karibu na vikundi hivyo pamoja na polisi kata ili kuhakikisha wahalifu wanadhibitiwa mapema kabla ya kusababisha madhara
Morogoro. Baada ya wakulima na wafugaji wa Kata ya Melela kuandamwa na matukio ya wizi wa mifugo kwa muda mrefu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeanzisha mkakati mpya wa ushirikishaji wananchi kwa kuunda vikundi sita vya ulinzi shirikishi vitakavyosaidia kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Hatua hiyo imeongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo ambaye amesema ushiriki wa wananchi katika ulinzi wa maeneo yao ni silaha muhimu ya kudhibiti uhalifu unaoendelea kuwasumbua wakazi wa Melela wilayani Mvomero.
Vikundi hivyo vimeundwa katika vijiji vinavyokaliwa na wakulima na wafugaji, ambavyo kwa muda vimekuwa vikikumbwa na matukio ya wizi wa mifugo na vitendo vingine vya kihalifu vinavyohatarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Baada ya uzinduzi wa vikundi hivyo, Kantimbo alikabidhi tochi 20 kwa wanavikundi hao ili kusaidia shughuli za doria na ulinzi nyakati za usiku, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa operesheni za kiusalama katika maeneo hayo.
Mmoja wa wafugaji akiwa na tochi baada ya kukabidhiwa na Jeshi la Polisi. Picha na Juma Mtanda
Akizungumza na wananchi wa Melela Kituoni leo Mei 4, 2026 wilayani Mvomero, Kamanda Kantimbo amesema viongozi wa vijiji na wananchi wanapaswa kushirikiana kwa karibu na vikundi hivyo pamoja na polisi kata ili kuhakikisha wahalifu wanadhibitiwa mapema kabla ya kusababisha madhara.
“Wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria vya uhalifu ili hatua zichukuliwe mapema. Ushirikiano wenu ni msingi mkubwa wa mafanikio katika mapambano dhidi ya wahalifu,” amesema Kantimbo.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mvomero, Boniface Mwakalyegese amewataka wananchi kuachana na utamaduni wa kumaliza kesi za uhalifu kimila kwa kulipana mifugo badala yake kufuata mnyororo wa sheria ili wahalifu wachukuliwe hatua stahiki.
Amesema baadhi ya matukio ya uhalifu yamekuwa yakifumbiwa macho kutokana na makubaliano ya kifamilia au kimila jambo linalochangia kuendelea kwa vitendo hivyo katika jamii.
Christopher Madukule, mfugaji wa eneo hilo aliyewawakilisha wananchi wenzake, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kusikiliza changamoto zao za kiusalama.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tunapata hasara kutokana na wizi wa mifugo, lakini hatua hii imetupa matumaini kuwa hali ya usalama itaimarika,” amesema Madukule.
Sauda Kipira, mkulima wa Melela, amesema mbali na kudhibiti wizi wa mifugo, vikundi hivyo vinapaswa kusaidia kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyowakumba watoto wa kike katika maeneo hayo.
Amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakikumbwa na vitendo vya ukatili wanapokuwa wakitumwa au wanapotembea umbali mrefu, hivyo uwepo wa vikundi vya ulinzi unaweza kusaidia kuongeza usalama wao.