Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Mbeya yafichua mtandao wa uhalifu, 987 wanaswa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akionyesha silaha zilizo kamatwa katika misako ya kukabiliana na uharifu mkoani hapa. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Mafanikio ya oparesheni hiyo yanaonesha juhudi za vyombo vya usalama katika kukabiliana na uhalifu, huku wito ukitolewa kwa wananchi kuwa macho na kutoa taarifa kwa wakati ili kudhibiti matukio kabla hayajatokea au kuleta madhara makubwa.

Mbeya. Katika hatua inayoonyesha ukubwa wa changamoto ya uhalifu mkoani Mbeya, Jeshi la Polisi limetangaza kukamata watu 987 wanaodaiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu ndani ya mwezi mmoja pekee, yakiwemo mauaji, ubakaji, ulawiti na wizi wa mali, zikiwemo vifaa vya makanisa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema watuhumiwa hao walinaswa kupitia oparesheni maalumu za misako na doria zilizofanyika kuanzia Aprili Mosi hadi 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti ongezeko la vitendo vya uhalifu katika mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 5, 2026, Kuzaga amesema oparesheni hizo zililenga makundi mbalimbali ya wahalifu waliokuwa wakijihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.

“Katika kipindi cha mwezi Aprili, tumefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 987 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji, kujeruhi, ubakaji, ulawiti, pamoja na kupatikana na silaha bila kibali na uvunjaji wa nyumba za ibada,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akionyesha kwa waandishi wa habari baadhi ya vifaa vilivyoibiwa kwenye nyumba za ibada na makazi ya watu jijini hapa.  Picha na Hawa Mathias

Katika moja ya matukio, Kamanda Kuzaga amesema polisi waliwakamata watu watatu wanaodaiwa kujihusisha na uwindaji haramu katika eneo la hifadhi.

Ametaja watuhumiwa hao kuwa ni Faustine Salesi (48), Nicolaus Lameck (32) na Daud Richard (33), wote wakazi wa Sikonge mkoani Tabora, waliokamatwa kati ya Aprili 19 na 23 katika Pori la Akiba la Piti lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

“Baada ya upekuzi, watuhumiwa walikutwa na vifaa mbalimbali, vikiwemo goroli 30, vipande vya vyuma vinavyotumika kama risasi pamoja na baiskeli. Uchunguzi wa awali unaonesha walikuwa wawindaji haramu,” amesema Kuzaga.


Wizi wa makanisani

Katika tukio lingine lililozua taharuki kwa waumini, watu sita wanashikiliwa kwa tuhuma za kuvunja na kuiba mali katika makanisa mawili yaliyopo eneo la Uyole, jijini Mbeya.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Athur Mwanza (28), Ayoub Mwaiswelo (42), Maski Mbulu (24), Isaya Isaya (27), Amadeo Alex (42) na Amos Amadeo (42), waliokamatwa katika mitaa ya Mwanyanje, Kinonde, Nyasi na DDC, Mbalizi.

Kuzaga amesema watuhumiwa hao walihusika na wizi katika makanisa ya Tanzania Assembly of God na Evangelistic Assemblies of God Tanzania, Ushirika wa Uyole.

“Walikutwa na vifaa mbalimbali vya muziki, ikiwemo spika, vipaza sauti, mixer, redio, pamoja na magodoro na vinywaji vikali,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo, mzee wa kanisa la EAGT Uyole, Paulo Mwampamba, amesema tukio hilo liliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za ibada.

“Tumepitia wakati mgumu sana baada ya kuibiwa vifaa vyetu. Tulilazimika kutumia njia mbadala kama kupiga madumu wakati wa ibada, lakini tunashukuru polisi kwa kufanikisha kuvipata tena,” amesema.

Hata hivyo, ametoa onyo kwa wahusika wa vitendo vya wizi kuacha mara moja, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi halali.

Mbali na matukio hayo, Kamanda Kuzaga amesema watu 15 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi kilo 3.19, pombe haramu (gongo) lita 160, sukari ya magendo kilo 40, mafuta ya kupikia lita 220 pamoja na mayai ya kuku yaliyoingizwa kinyume cha sheria kutoka nchi jirani.

Amesema oparesheni hizo zinaendelea na zitakuwa endelevu ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama dhidi ya vitendo vya uhalifu.


Kesi 324 zafikishwa mahakamani

Kuhusu hatua za kisheria, Kuzaga amesema katika kipindi hicho, jumla ya kesi 324 zilifikishwa mahakamani, ambapo kati ya hizo, kesi 130 zimekamilika na watuhumiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali, huku kesi 164 zikiendelea katika hatua tofauti za kisheria.

Muonekano wa vitu vya wizi vilivyo kamatwa na Jeshi la Polisi kwa watuhumiwa wa matukio ya uharifu katika kipindi cha mwezi Aprili, mwaka huu. Picha na Hawa Mathias

Miongoni mwa kesi zilizovuta hisia za wengi ni ile ya mkazi wa Stamico, wilayani Chunya, Dida Lupia (36), aliyepatikana na hatia ya kumbaka na kumlawiti mtoto wa miaka nane.

Mahakama ya Wilaya ya Chunya, chini ya Hakimu James Mhanuzi, ilimhukumu kifungo cha maisha jela baada ya kuthibitishwa kosa hilo.

Katika hatua nyingine, wananchi wameitaka polisi kuongeza juhudi za utoaji elimu kwa jamii ili kushirikiana kikamilifu katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Mkazi wa Mbeya, Janeth Haule amesema ipo haja ya kuimarisha ulinzi shirikishi hasa katika maeneo yenye ongezeko la vitendo vya wizi wa rejareja.

“Wananchi tunapaswa kushirikishwa zaidi katika ulinzi wa maeneo yetu. Vibaka wamekuwa wengi, hivyo elimu ni muhimu ili tuweze kujilinda na kusaidiana na vyombo vya dola,” amesema.

Jeshi la Polisi mkoani humo limewahakikishia wananchi kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wahalifu, likisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kuhakikisha usalama wa kudumu.