PIC yawatimua Wakala wa Vipimo

Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma(PIC).
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imeshindwa kutoa maelekezo kwa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), baada ya bodi ya wakurugenzi kumaliza muda wake.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imewatimu viongozi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) baada ya wakala huo kukosa bodi ya wakurugenzi.
Akizungumza leo Alhamisi, Januari 19,2023, Mwenyekiti wa PIC, Jerry Silaa amesema wakala hao walifika katika kamati hiyo lakini bodi yao ilikuwa imemaliza muda wake tangu Juni 2021.
Amesema baada ya bodi kumaliza muda wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara alipaswa kukaimu madaraka kwa muda usiozidi mwaka mmoja, muda ambao pia umemalizika Juni mwaka jana.
“Kwa hiyo Wakala wa Vipimo nchini tumeshindwa kupokea taarifa yake na kufanya vikao vyake kwasababu walikuja bila bodi na kama huwa inatoa maelekezo kwa bodi ya taasisi,”amesema.
Amesema iwapo bodi ya taasisi haipo kamati haiwezi kupokea taarifa wala kutoa maelekezo na ndio maana waliamua kutofanya uchambuzi wa wakala huo.
“Tumewarejesha wakala wa vipimo hadi pale tutakapowaita tena baada ya kutaarifiwa kuwa wameweza kuunda bodi,”amesema.
Aidha Silaa alisema kutokana na uwepo wa mashine nyingi za michezo ya kubahatisha nchini zinazofanya kazi bila kusajiliwa, kamati imeitaka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kutoa elimu.
“Natoa wito kwa Watanzania wanapoona mashine yoyote ya mchezo ya kubahatisha ambayo haina stika ya bodi ya michezo ya kubahatisha kutoa taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa,”amesema Silaa ambaye pia Mbunge wa Ukonga (CCM).