NSSF yalipa mafao ya Sh56.68 bilioni kwa miezi sita

Muktasari:
- Matumizi ya mifumo ya Tehama imetajwa kuwa kichocheo cha kuiwezesha NSSF kulipa wastaafu kwa wakati
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umelipa Sh56.689 bilioni za mafao ya wastaafu katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2023.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omari Mziya amesema hayo leo Februari 15,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam.
Pia, amesema mfuko umeandaa mpango mahususi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wanachama na tayari mpango huo unaendelea kutekelezwa kwenye ofisi mbalimbali za NSSF kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Mziya amesema NSSF inawathamini wanachama wake, hivyo inawaomba waajiri wote wa sekta binafsi kutimiza wajibu wao kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi ili kuwaondolea usumbufu watakapostaafu waweze kulipwa mafao yao kwa wakati.
Amesema mfuko unaendelea kulipa pensheni kwa wastaafu na Januari 2024, imelipa Sh 9.93 bilioni.
"NSSF tunajivunia kuwa na wastaafu ambao tunawalipa kwa wakati kila inapofika tarehe 25 ya kila mwezi, dhamira na lengo letu ni kuona wafanyakazi wote katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wanaingia katika malipo ya pensheni ili kupunguza umasikini utokanao na uzee au kukosa kipato," amesema Mziya.
Amesema mfuko huo upo katika uhakiki wastaafu ulioanza Februari mosi na utaendelea mpaka Aprili 30, 2024 akiwataka wastaafu na wategemezi kutumia muda huo kufanya uhakiki kwenye ofisi zote za NSSF zilizopo Tanzania Bara na waliopo Zanzibar wafike katika ofisi za ZSSF.
Akizungumzia huduma za mfuko huo, Mzee Nicholas Kingazi ambaye ni mkazi wa Tabata amesema anafurahishwa na huduma zinazotolewa kwa wazee wastaafu, huku wasiojiweza wamekuwa wakifuatwa majumbani kwa ajili ya kuhakikiwa taarifa zao.
"Nimefarijika sana kwa sababu kitendo mlichokifanya NSSF cha kufuata wazee wasiojiweza kuwahakiki majumbani kwao," amesema Mzee Kingazi.