NMB yazindua klabu ya mwanamke jasiri mkoani Mtwara
Muktasari:
Benki ya NMB Kanda ya Kusini imezindua klabu ya mwanamke jasiri ikiwa ni jitihada za kumuinua mwanamke kiuchumi.
Mtwara. Benki ya NMB Kanda ya Kusini imezindua klabu ya mwanamke jasiri ikiwa ni jitihada za kumuinua mwanamke kiuchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hiyo meneja wa NMB Kanda ya Mtwara, Janeth Shango amesema ili kumuinua mwanamke, benki hiyo imetoa fursa kwa makundi mbalimbali ya wanawake waweze kupata mikopo.
Amebainisha kuwa vikundi hivyo vitakavyojiunga na klabu hiyo vitapewa kipaumbele cha kupata mikopo ya kuendesha biashara zao.
"Hii klabu tumeianzisha ili iweze kumsaidia mwanamke kwenye kila nyanja kuwezesha wanawake kujikwamua kiuchumi. Tumefanya hivi ili kumsaidia mwanamke aweze kushiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali.”
"Kupitia NMB Mwanamke jasiri tunaamini kuwa tunahamasisha wanawake wapate mikopo yenye riba nafuu itakayowawezesha kuendesha maisha yao kikubwa ni uaminifu na uadilifu kopeni kwa ajili ya biashara,” amesema Shango.
Naye mkuu wa maendeleo manispaa ya Mtwara, Juliana Manyama amesema wanawake wengi ndio walezi wa familia wanaweza kupata mikopo na wakainuka kiuchumi.
"Leo nimeondoka na funzo kubwa kumbe ninaweza kuwaelewesha wanawake wenzetu wakapata mikopo itakayowasaidia kukuza uchumi fursa zipo nyingi kupitia hii programu ya mwanamke jasiri wanawake wanapaswa wanyanyuke na kuona umuhimu wa kukuza vipato vyao.”
"Wanawake tumepewa fursa tunapaswa kuwa na nidhamu ya biashara na fedha, unajua wanawake wengi wamekuwa wakilazimika juu ya mitaji na wanahangaika kufanya biashara zisizokua lakini kupitia mwanamke jasiri inaweza kutusaidia zaidi," amesema Manyama.