NHC yaweka rekodi ujenzi wa nyumba

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu akizungumza kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili jijini Dar es salaam juzi. Picha na Emmanuel Herman
Muktasari:
- Kwa miaka mitano imejenga nyumba zaidi ya 8,000 ikiwa ni nusu ya nyumba ambazo zilijengwa kwa miaka 50.
Dar es Salaam. Shirika la nyumba (NHC) limeweka historia kwa kujenga nyumba zaidi ya nusu ya zilizojengwa kwa miaka 50 iliyopita ndani ya kipindi cha miaka mitano tu.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake juzi, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu alisema kuanzia mwaka 2010 hadi sasa wameshajenga nyumba 8,800 za biashara na makazi ya bei nafuu.
“Tangu mwaka 1962 shirika hili lilipoanzishwa hadi mwaka 1972 au 1974 lilijenga nyumba 14,000 ambazo sehemu kubwa ya bajeti ya miradi ilikuwa ikitolewa na Serikali. Lakini tangu mwaka 2010 nilipoingia mimi hadi sasa, NHC imefanikiwa kujenga nyumba 8,800 zikiwamo za bei nafuu na zote zimenunuliwa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kasi ya ujenzi wa nyumba hizo miaka ya 1970 ilishuka kutokana na nchi kukumbwa na mtikisiko wa uchumi uliochangiwa na mfumuko wa bei ya mafuta na kujitoa kwa Ujerumani Mashariki kuchangia sekta hiyo.
“Ukichukua kipindi cha 1976 hadi 2010 – wakati Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alipoamua kufanya mageuzi ya NHC – nyumba tulizokuwa tumejenga NHC zilikuwa hazifiki 2,000 zikihusisha miradi mikubwa ya nyumba za Boko nyumba 250, Mbweni (50), na Mbezi nyumba 30 zilizopo jijini Dar es Salaam,” alisema.
Kwa mahesabu yaliyofanyika kutoka 1990 hadi mwaka 2012, shirika hilo lilikuwa limejenga nyumba 458 kiwango alichoeleza kuwa ni kidogo kwa maendeleo ya makazi nchini. Baada ya yeye kuongoza mageuzi, NHC imefanikiwa kujenga nyumba 8,800 nchini kati ya hizo za bei nafuu zikiwa ni 3,000 katika mzunguko wa kwanza wa miradi yao.
Hata hivyo, alisema nyumba hizo ni pungufu ya malengo yaliyopo kwenye mpango mkakati wa mwaka 2010-2015 wa kujenga nyumba 15,000 kwa miaka mitano, yakiwamo makazi ya bei nafuu 5,000.
Mchechu alisema kuwa wanapojenga hulenga hali za watu; wa kipato cha chini, cha kati na juu, na au wafanyabiashara wa kati na wa juu. Lengo la NHC, alisema ni kuchangia kuwapa wananchi makazi bora na nafuu zaidi.
Alipoulizwa juu ya tuhuma kuwa nyumba zinazojengwa na NHC hazinunuliki, Mchechu alisema nyumba zote za bei nafuu zimeshanunuliwa na kwamba nyingi hununuliwa hata kabla ya kukamilika kujengwa.
“Hakuna nyumba ambazo zimedoda. Ukitaka kulinganisha basi ufanye kuwa kwa kutumia vigezo sawa kote yaani kama nyumba za vyumba viwili vya kulala za NHC basi iwe hivyo kwa mashirika mengine. Kama ni vyumba vitatu iwe hivyo pia kwa mashirika mengine. Nyumba zetu zimenunuliwa kwa sababu bei ni ya chini kuliko mashirika yote ya ujenzi unayoyajua,” alisisitiza.
Kuhusu vyanzo vya fedha, Mkurugenzi huyo alisema kwamba kati ya mwaka 1962 na katikati ya mwaka 1970 sehemu kubwa ya bajeti ya miradi ilikuwa ikitolewa na Serikali kwa asilimia 45, NHC asilimia 13, na asilimia 42 ilikuwa ikichangiwa na Serikali ya Ujerumani Mashariki. Lakini hivi sasa miradi yote inajengwa kutokana na fedha zinazotokana na shirika lenyewe.
Mchechu alisema baada ya kuingia mkataba wa miaka minne mwaka 2010 alifanya uamuzi mgumu kulirudisha shirika hilo katika ufanisi ikiwamo kuvunja mikataba ya kilaghai ya upangishaji nyumba ambapo baadhi ya vigogo na watumishi wa NHC walikuwa wakichukua nyumba na kupangisha.
Pia, alisema aliamua kuanzisha utaratibu mahususi wa utafutaji fedha kwa kukopa katika benki kwa riba ya wastani wa asilimia 15 ili kugharamia miradi mikubwa kwa kuwa shirika lilikuwa halina fedha za kutosha. Utaratibu huo umeliwezesha shirika kuwekeza Sh600 bilioni katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na kati ya fedha hizo, mikopo ni Sh240 bilioni.
“Nilipoingia mapato ya shirika yalikuwa Sh36.6 bilioni mwaka 2010 lakini baada ya maboresho ya kuongeza ufanisi na utekelezaji wa miradi mbalimbali mapato hayo yameongezeka hadi kufikia Sh130 bilioni mwaka 2014,” alisema.
Katika mchanganuo huo, alisema faida imeongezeka hadi kufikia Sh27.3 bilioni mwaka jana ikilinganishwa na faida ya Sh3.1 bilioni aliyoikuta mwaka 2010.