Nafuu kwa waishio mabondeni, maeneo yenye ardhi oevu

Muktasari:
- Watafiti barani Afrika wakutana kujadili mbinu za kukabiliana na athari za mafuriko na kushirikishana namna ya kuendeleza miji inayosumbuliwa na athari za mvua na ardhi oevu.
Dar es Salaam. Kama moja ya miji inayoongoza kwa ukuaji haraka barani Afrika, Dar es Salaam inakabiliana na changamoto kutokana na mabadiliko ya haraka ya miji na ya tabianchi.
Miongoni mwa changamoto hizo ni athari za hali ya hewa yakiwamo mafuriko yanayoathiri maisha, miundombinu na shughuli za kiuchumi.
Wataalamu wanabainisha kama ilivyo miji mingine ya pwani, Dar es Salaam inakabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa kina cha maji baharini, mvua za mara kwa mara husababisha mafuriko, kuhama kwa watu na kuharibu miundombinu muhimu.
Watafiti na wataalamu wa mipango miji wameanza tafiti za namna bora ya kuongeza ustahimilivu wa miji ya Afrika, kuhakikisha inabaki kuwa vituo vya kiuchumi na mazingira bora kwa wakazi wake.
Katika kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Afrika cha Masomo ya Miji Endelevu chini ya mada isemayo: “Njia mpya za maendeleo ya miji imara na endelevu barani Afrika” wataalamu, watunga sera, na watafiti kutoka nchi 16 walikusanyika jijini Dar es Salaam jana Februari 27, 2025 kujadili suluhisho kuhusu miji iliyo pembezoni mwa maji kama vile Dar es Salaam.
Mtafiti kutoka Nigeria anayesimamia mradi wa African Water Cities, Kunle Adeyemi amesisitiza haja ya kukabiliana kwa haraka na mabadiliko ya hali ya hewa ili kudumisha miji ya Afrika.
“Miji yetu inazama. Katika siku za usoni watu wataishi zaidi juu ya maji na miji ya Afrika kama Dar es Salaam itakuwa katikati ya mabadiliko haya,” amesema.
Katika utafiti aliofanya anasisitiza mbinu za ubunifu zinazojumuisha maarifa ya asili katika mipango miji.
Ametoa mfano wa mradi wa Makoko uliotekelezwa mjini Lagos, Nigeria ambao umeonyesha namna nyumba zinavyoweza kujengwa hata kwenye maeneo yenye ardhi oevu.
Adeyemi amesema mikakati kama hiyo inaweza kutumika katika miji mingine kama Dar es Salaam kuzuia mafuriko ambayo kwa kiasi kikubwa husababisha uharibifu wa ardhi.
“Tunahitaji kufikiria upya muundo wa miji ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi. Hii inamaanisha kujumuisha suluhisho za msingi wa maji ambazo zinaweza kustahimili kuongezeka kwa mawimbi na hali ya hewa kali,” amesema.
Mpango mahususi wa kukabiliana na changamoto hizo amesema ni mradi wa utafiti wa miaka 10 unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji kwa gharama ya Euro milioni sita (sawa na Sh16.2 bilioni).
Mradi huo unaoshirikisha vyuo vikuu vinne vya Ubelgiji na Chuo Kikuu Ardhi cha Tanzania, unalenga kuongeza uwezo wa nchi za Afrika kusimamia maendeleo ya miji yenye ustahimilivu.
Kupitia mpango huo, amesema wataalamu 44 wa Tanzania watapewa Shahada za Uzamivu (PhD) na 25 wengine Shahada za Uzamili katika mipango ya miji na ustahimilivu wa tabianchi.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Hasselt cha Ubelgiji, Profesa Bernard Vanheusden amesema mradi huo unalenga kukuza ushirikiano kati ya wataalamu na watunga sera.
“Tunaweza kuunda mikakati bora ya mipango miji inayozuia matatizo kama vile makazi yasiyo rasmi na miundombinu isiyofaa,” amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Evaristo Liwa amesema kuna umuhimu wa kufanya uchambuzi kuhusu mipango miji.
“Hatua ya kwanza katika kukabiliana na changamoto za miji ni uchambuzi wa data, ambao unawawezesha watafiti na watunga sera kutabiri ukuaji wa miji na kupanga,” amesema Profesa Liwa.
“Tafiti nyingi zimefanyika lakini changamoto bado zipo kwa sababu hakujawa na umakini mkubwa katika mipango miji ya muda mrefu. Tunahitaji kuchambua data za maendeleo ya miji katika miaka 50 ijayo ili kuongoza mabadiliko ya kisheria na sera,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Daniel Mushi amesema ipo haja ya tafiti zinazofanyika kuingizwa kwenye sera kwa ajili ya utekelezaji.
“Moja ya changamoto kubwa katika mipango miji ni kuhakikisha matokeo ya utafiti na mapendekezo ya sera yanabadilika kuwa mikakati inayotekelezeka,” amesema.
Dk Mushi amesema maono ya Tanzania 2025 yanatarajia uchumi wa kati, wenye viwanda na miji iliyo na maendeleo.
“Ili kufikia hili, lazima tuhakikishe miji yetu siyo tu injini za uchumi bali pia kuwa na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na endelevu kwa wananchi wote,” amesema.