Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanafunzi kidato cha nne adaiwa kujinyonga hadi kufa kwa waya

Mkazi wa mtaa Nyakanyasi kata Bakoba manispaa ya Bukoba Mkoa wa Kagera, Mama mzazi wa (Kareni), Rose Fadhili akisimulia jinsi alivyokuta mwanawe amejinyonga kwa kutumia waya.

Muktasari:

  • Akutwa amejinyonga kwa kutumia waya kwenye chumba kimojawapo cha nyumba iliyokuwa ikijengwa nyumbani kwao, chanzo ikisadikika kulazimishwa kusoma na kupelekwa shule na mama yake.

Bukoba. “Kareni mwanangu, sikuwahi kugombana naye zaidi ya masuala ya masomo. Alikuwa na ndoto nyingi, aliniahidi mambo mengi ya kubadilisha maisha yangu."

Hayo ni maneno ya Rose Fadhili, mkazi wa mtaa wa Nyakanyasi Mlimani katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, aliyoyatamka kwa uchungu huku akibubujikwa machozi, wakati akizungumza na Mwananchi Digital leo, Alhamisi Aprili 10, 2025, kutokana na kifo cha mwanaye, Kareni Mwemezi (18), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kagemu. Kareni  amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia waya, tukio hilo likihusishwa na mzozo baina yake na mama yake kuhusu kwenda shule.

Mama mzazi wa Kareni, Rose Fadhili akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi kuhusiana na kifo hicho cha mwanaye, amesema kabla ya tukio, walikuwa na mazungumzo kuhusu tabia yake ya kupendelea kwenda kwenye vibanda vya kuweka muziki na kucheza michezo ya bonanza, badala ya kuhudhuria masomo.

"Alikuwa na kawaida ya kwenda kwenye vibanda hivyo. Nilipokuwa nikimuuliza, alinijibu kuwa anafanya anachokifahamu, akanitaka nimuache," amesema Rose.

Akiendelea kueleza, amesema jana Jumatano, Aprili 9, 2025, aliporudi nyumbani kutoka kazini, hakumkuta na alipohoji wapi alipo akamwambia yuko mtaani, “nilipomuuliza kuhusu shule, alinijibu ameenda na amerudi.”

Mama huyo anasema usiku alizungumza na mwanaye kwa kina na alimshauri aachane na makundi mabaya kwa sababu yanampotosha na badala yake ajikite kwenye masomo.

“Wakati namsema nilimpa adhabu ndogo ya kumfinya masikio, akaniomba msamaha, tukala chakula na baadaye tukasali kwa pamoja kisha tukalala,” amesimulia.

Amesema leo asubuhi (Aprili 10), alimwambia Kareni hatamruhusu kwenda shuleni peke yake, bali atampeleka mwenyewe ili akazungumze na walimu kuhusu maendeleo yake.

“Kareni alinikubalia, akasema sawa mama tunaenda wote,” amesimulia mama huyo kwa uchungu.

Rose anasema aliingia chumbani ili ajiandae kuelekea shuleni na mwanaye, lakini alipotoka ili waondoke hakumkuta sebuleni.

Anasema alimuita lakini hakuitika na mara akasikia kishindo kama mtu anapita nyuma ya nyumba yao na alipotoka nje, hakuona mtu yeyote na mwanaye pia hakuwepo.

“Nikaamua kwenda kwa mwenyekiti wa mtaa  kumweleza, kisha nikapita njia ya pili nikitazamia kumkuta kwenye vibanda, lakini sikumkuta. Niliporudi nyumbani, nilielezwa na majirani pamoja na mwenyekiti kuwa Kareni amekutwa amejinyonga. Sikutaka kuamini. Nilipoenda kuchungulia ndani ya chumba ambacho kilikuwa hakijakamilika kujengwa, nilimkuta akiwa amejitundika kwa kutumia waya," amesimulia mama huyo kwa uchungu.

Mwananchi imemtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda kuhusiana na tukio hilo, ambapo alijibu kuwa  yupo nje ya mji kikazi lakini bado hajapokea taarifa ya kifo hicho na akiipata ataitolea maelezo.

Jirani yake Rose aliyejitambulisha kwa jina la  Rameck Paulo amesema asubuhi alienda nyumbani kwa Kareni kuchukua mashine ya kufyatulia tofali, lakini alipoita hakuna mtu aliyeitika.

Amedai alipozidi kusogea alimuona mtu amejitundika kwenye moja ya chumba kinachojengwa na hakijakamilika.

Lakini amedai aliposogea jirani zaidi, alibaini ni Kareni amejitundika ndipo akatoa taarifa kwa majirani na kwa mwenyekiti wa mtaa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa huo wa Nyakanyasi, Anord Ngilwa amekiri  kupokea taarifa ya Kareni kutohudhuria shuleni kutoka kwa mama yake.

“Nilimshauri aendelee kumtafuta aende naye shuleni ili akafahamu zaidi nini kinachoendelea, lakini baada ya muda mfupi nikapigiwa simu na majirani zake walioniambia Kareni amejinyonga nyumbani kwao,” amesema.

Amesema alitoa taarifa Polisi ambao walifika na kuuchukua mwili na kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba kwa uchunguzi zaidi.

Mwenyekiti huyo amesema tukio hilo ni la tatu mtaani hapo la mtu kujinyonga ndani ya mwaka huu.