Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu mkuu, walinzi mbaroni tuhuma za mauaji ya mwanafunzi

Muonekano wa majengo ya shule ya St Kagwa

Muktasari:

  • Mwalimu mkuu na walinzi wawili mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha nne. Ilidaiwa kuwa wanafunzi hao baada ya kuruka ukuta waliingia kwenye bweni la wasichana na ndipo walipokamatwa na walinzi na kuanza kupigwa.

Rukwa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi wa kidato cha nne, Novatus Adelhard Mgeni (15), ambaye alifariki dunia katika shule ya Sekondari Kagwa iliyopo Manispaa ya Sumbawanga.

Akitoa taarifa ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, SACP Justin Masija amesema kuwa Machi 23, 2025, saa 8:00 usiku, watuhumiwa watatu walimshambulia mwanafunzi Novatus Mgeni pamoja na wanafunzi wenzake wawili kwa kuwapiga kwa kutumia waya.

Kwa mujibu wa Masija tukio hilo lilitokea katika Shule ya Sekondari Kagwa, iliyopo Manispaa ya Sumbawanga.

Masija amewataja waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni mkuu wa shule hiyo, Zacharia Mwasenga (45) na walinzi wawili wa shule hiyo, Michael Donasio (33) na Geofrey Simon (30).

Amesema uchunguzi wa tukio unaendelea na polisi wanaendelea kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya watuhumiwa.

Kwa mujibu wa taarifa wanafunzi walipigwa kwa  kutuhumiwa kuruka uzio wa ukuta inayotenganisha shule mbili yaani Kagwa Sekondari na St Kagwa Sekondari.

Ilidaiwa kuwa wanafunzi hao baada ya kuruka ukuta waliingia kwenye bweni la wasichana na ndipo walipokamatwa na walinzi na kuanza kupigwa.

Wanafunzi hao baada ya kushambuliwa walifikishwa Kituo cha Polisi Sumbawanga na hatimaye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga.

Wanafunzi wawili walitibiwa na kuruhusiwa isipokuwa Novatus ambaye hali yake ilizidi kuwa mbaya na hivyo akahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ambapo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.

Kamanda Masija amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wawafikishe watuhumiwa kituoni ili kuendelea na hatua nyingine.

Amesema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mbele mkono wa sheria pindi uchunguzi utakapokamilika.