Mv Kigamboni kufanyiwa ukarabati mkubwa

Kivuko cha MV Kazi kikiendelea kutoa huduma ya uvushaji Kigamboni-Magogoni. Picha na Mpigapicha wetu
Muktasari:
- Temesa imesitisha huduma za kivuko cha Mv Kigamboni kuanzia Juni 7, 2024 kwa ukarabati. Abiria wameshauriwa kutumia Daraja la Mwalimu Nyerere. Hata hivyo, Mv Kazi pekee ndiyo inatoa huduma, na abiria wengine wanatumia boti za wavuvi.
Dar es Salaam. Hatimaye Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) umetangaza kusitisha huduma za uvushaji abiria kwa kutumia kivuko cha Mv Kigamboni kuanzia leo Ijumaa Juni 7, 2024.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Temesa, inalenga kwenda kukifanyia ukarabati mkubwa kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Kigamboni-Magogoni jijini Dar es Salaam.
Uamuzi wa Temesa umefikiwa wiki moja tangu gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii lichapishe ripoti maalumu kuhusu changamoto za vivuko katika eneo la Kigmboni-Magogoni.
Ripoti hiyo ilibainisha kivuko cha Mv Kigamboni kimepitiliza muda wa ukarabati mkubwa, lakini kinaendelea kutoa huduma, hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji.
Ripoti pia iliweka wazi kuwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) lilishakisimamisha kivuko hicho kutoa huduma kulinda usalama wa watumiaji, lakini bado kiliendelea kutumika.
Kivuko chasitishwa
Taarifa ya kusitishwa huduma kwa kivuko hicho ilitolewa Alhamisi Juni 6, 2024 na Temesa kupitia kitengo cha Masoko na Uhusiano.
Taarifa hiyo imewashauri abiria wenye magari kwa sasa kutumia njia mbadala ya Daraja la Mwalimu Nyerere, eneo la Kurasini ili kuepusha msongamano Magogoni, hadi pale Mv Kigamboni kitakaporejea.
"Aidha, shughuli za uvushaji katika eneo hilo, zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa kutumia kivuko cha Mv Kazi na Sea Tax," imeeleza taarifa hiyo.
Temesa kupitia taarifa hiyo, inawaomba radhi abiria wote kutokana na usumbufu watakaoupata wakati wote ambao kivuko cha Mv Kigamboni hakitakuwepo.
Hali ya huduma
Licha ya magari kutakiwa kutumia njia mbadala ya Daraja la Mwalimu Nyerere, bado katika eneo hilo leo kumeshuhudiwa magari yakivushwa.
Taarifa ya Temesa imeeleza huduma zitaendelea kutolewa na Mv Kazi na Sea Tax, lakini Mwananchi imeshuhudia hali tofauti leo asubuhi.
Ni kivuko cha Mv Kazi pekee ndicho kilichoonekana kikivusha abiria tangu saa 1:07 asubuhi Mwananchi ilipofika eneo hilo. Hakuna Sea Tax iliyoonekana ikifanya kazi muda huo.
Kivuko kimoja cha Sea Tax kilishuhudiwa kikiwa kimeegeshwa upande wa Magogoni (Posta) sambamba na kivuko cha Mv Kigamboni kinachotarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Kutokana na huduma kutolewa na kivuko cha Mv Kazi pekee, idadi kubwa ya abiria ilikuwapo hasa upande wa Kivukoni ikisubiri huduma.
Kivuko hicho kimejaza zaidi abiria kila kilipotokea upande wa Kivukoni (Kigamboni) na kilipakia abiria wachache pale kilipotoka upande wa Magogoni (Feri).
Hiyo inatokana na abiria kutoka Kigamboni kuwa wengi muda wa asubuhi kwenda Posta zilizo shughuli nyingi, baadhi yao wakienda kwenye soko la samaki Feri kwa shughuli za kibiashara.
Kwa kawaida, jioni mambo hubadilika na abiria wengi huwa upande wa Magogoni wakitoka makazini kurudi nyumbani Kigamboni.
Boti za wavuvi kuvusha abiria
Kutokana na uchache wa vivuko, baadhi ya abiria walishuhudiwa wakipanda boti za wavuvi kuvushwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Kupitia boti hizo, abiria walitozwa Sh1,000 kuvushwa na hata hivyo wanadai wanatumia muda mfupi kuliko kusubiri kivuko cha Mv Kazi pekee, ambako hutozwa Sh200.