Mtoto wa Askofu aliburuza kanisa mahakamani

Muktasari:
- John Sepeku alikuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam na pia Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, akihudumu kuanzia Julai 5, 1970 hadi alipojiuzulu Septemba Mosi 1978.
Dar es Salaam. Bernardo Sepeku ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, amelishtaki kanisa hilo mahakamani akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa na baba yake mwaka 1978.
Bernardo amefungua shauri namba 378/2023 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sosthenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam, na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Katika shauri hilo ambalo liko mbele ya Jaji Arafa Msafiri, mdai anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 kilichopo Buza, Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa Askofu Sepeku kama zawadi.
Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake, ameiomba Mahakama hiyo iamuru kanisa hilo kuzingatia azimio lao, lililopitishwa na taasisi yao ili kumuwezesha kuandika na kuorodhesha mali za baba yake Askofu Sepeku wakati shauri hilo lilipokuja Novemba 30, 2023 kwa ajili ya kutajwa.
Pia, ameiomba Mahakama hiyo imuamuru Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, Askofu Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd kwa pamoja kulipa Sh33 milioni ikiwa ni hasara aliyoipata mlalamikaji kutokana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika shamba lililoko ndani ya kiwanja hicho.
"Waumini wa Dayosisi ya Dar es Salaam walimpa zawadi kwa kazi nzuri na upendo waliokuwa nao Askofu Sepeku mwaka 1978 na baadaye kuidhinishwa na Mkutano Mtakatifu wa Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ya Kanisa la Anglikana, katika kikao chake cha sinodi kilichofanyika mwaka 1980, kiliamua kutoa zawadi," amedai Bernardo.
Mlalamikaji huyo pia amedai mazao yaliyoharibiwa shambani ni miti ya michungwa, minazi, mihogo, miti ya mipapai, miti ya malimao na miembe.
Pia mlalamikaji huyo anataka alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi iliyopo katika kiwanja hicho na wanaomba fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Februari 12, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji.
Inadaiwa kuwa Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kushirikiana na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam limechukua kiwanja hicho na kumpatia Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.