Msekwa asimulia siku tano za moto kabla ya muungano

Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa katika moja ya mahojiano. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar, walisimama imara kuhakikisha kwamba wanaunganisha mataifa yao na kuimarisha undugu na mshikamano.

Zikiwa zimebaki siku mbili kwa Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa amesimulia siku tano muhimu kuelekea muungano wa Aprili 26, 1964.

Msekwa ni mmoja wa viongozi waliohusika moja kwa moja katika kufanikisha Muungano huo, kwani kwa nafasi yake ya Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo, alikuwa kiungo muhimu katika kufanikisha hilo.

Mwanasiasa huyo mstaafu amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi, akielezea siku hizo tano, kuanzia Aprili 22, 1964 hadi Aprili 26, 1964, zilivyokuwa muhimu katika kufanikisha muungano huo ambao unafikisha miongo sita sasa.

Msekwa anasema kuanzia hatua ya maridhiano hadi kukamilika kwa Muungano wenyewe, vilifanyika kwa haraka ndani ya siku tano pekee na muungano huo ukafanyika siku ya kilele, Aprili 26, 1964.

Waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar, walisimama imara kuhakikisha kwamba wanaunganisha mataifa yao na kuimarisha undugu na mshikamano.

Anasema kila ifikapo Aprili 26, Watanzania wanasherehekea maadhimisho ya Muungano, lakini ambacho wengi hawakifahamu ni kwamba, muungano huo ulikamilika Aprili 25, 1964, lakini uhai wake ukaanza Aprili 26, mwaka huohuo.

Akifafanua hilo, Msekwa anatolea mfano uhai wa binadamu ambao anautaja kuwa tofauti na wa sheria, kwamba uhai wa binadamu unaanza wakati ule ule mtoto anapozaliwa lakini uhai wa sheria una utaratibu tofauti.

“Unaweza kuanza palepale sheria inapokamilisha taratibu zake zote na kupitishwa na Bunge na kuridhiwa na Rais au ukaanza badae kutegemea na tamko lenyewe.

“Wakati ule sheria iliyounda Muungano ilisema kwamba uhai wake utaanza siku inayofuata mara baada ya kuridhiwa na Bunge,” anasema Msekwa.

Anaeleza kuwa sheria hiyo iliridhiwa na Bunge Aprili 25, 1964 na ikatamka uhai wa Muungano utaanza siku inayofuata (Aprili 26).

“Ndio maana huwa tunasherehekea maadhimisho yake siku hiyo, ingawa mabunge mawili; Bunge la Tanganyika likishirikiana na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar yaliridhia Muungano huo siku moja kabla,” anasema.

Spika huyo mstaafu anasema, wakati huo alikuwa ni Katibu wa Bunge, nafasi aliyoanza kuitumikia tangu mwaka 1962.

“Kwa kuwa sheria zinapitishwa na Bunge, mimi ndiyo nilikuwa katikati ya matukio yote hayo, wakati hili la Muungano linatokea, kilikuwa ni kipindi ambacho Bunge limeahirishwa, halikuwa kwenye kikao.

“Ikabidi wabunge waitwe kwa dharura Dar es Salaam ili waje kwenye kikao cha kupitisha sheria hiyo,” anasema.

Anasema lilikuwa ni jambo la haraka, hiyo ni baada ya makubaliano ya Rais wa Tanganyika (Nyerere) na Rais wa Zanzibar (Karume).

Msekwa anasema makubaliano ya marais hao yalisainiwa Aprili 22, 1964 lakini kwa kuwa yalikuwa ni makubaliano ya kimataifa, yasingeweza kupata uhai bila kuridhiwa na mabunge ya nchi zinazohusika (Tanganyika na Zanzibar).

“Ndipo mabunge hayo mawili yakaitwa kwa ajili ya kikao cha dharura ili kuridhia mkataba huo, hayo yote yalifanyika haraka, kuanzia mapatano ya wakubwa (Nyerere na Karume), Aprili 22, hadi Aprili 25 wabunge waliporidhia, ndipo ikazaliwa nchi ya Tanzania na uhai wa Muungano ukaanza Aprili 26, 1964,” anasema.


Sababu za kufanya haraka

Msekwa anaeleza kuwa kulikuwa na sababu mbili kubwa zilizosababisha uharaka wa jambo hilo ambazo pia zilifanyika kwa siri.

“Ilikuwa lazima ufanyike kwa siri, maana maadui wa Muungano walikuwepo wakati ule na wasingependa nchi hizi ziungane.

“Mwalimu Nyerere alikuwa na kumbukumbu ya namna Muungano wa Nchi za Afrika Mashariki ulivyoshindikana.

Anasema mwaka mmoja kabla ya Muungano huo (1963), marais wa Tanganyika, Kenya na Uganda walikutana jijini Nairobi, wakatangaza Muungano wa Shirikisho la Afrika Mashariki kwamba ungeundwa mwisho wa mwaka huo.

“Hilo lilitangazwa rasmi, lakini kutokana na sababu ambazo hatuzijui lilishindikana, kwa hofu hiyo na kwa upande wa Rais Karume ilikuwa ni kipindi ambacho ametoka kuipindua Serikali ya Waarabu, hivyo kulikuwa na wasiwasi kwamba wale wanaweza kutamani kurudi kumpindua yeye (Karume),” anasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, anasema kutoka na hofu hizo mbili, ilibidi jambo la Muungano lifanyike kwa usiri na kwa haraka kwa kuwa hata kwa Zanzibar kulikuwa na hofu ya Serikali ya Mwarabu kurudi.

Zanzibar ilifanya Mapinduzi, Januari 12, 1964 kipindi ambacho Msekwa anasema hawakuwa wameunda jeshi, hawakuwa na nguvu za kupambana endapo Waarabu wangerudi kumpindua Karume.

“Kulikuwa na wasiwasi kwamba Zanzibar inaweza kushambuliwa na Waarabu, hivyo suala la Muungano likapewa umuhimu kwamba Wazanzibari wakiungana na Watanganyika watakuwa na nguvu ya kupambana na shambulizi la namna hiyo kama lingetokea.

“Sababu hizo zilifanya jambo hili lifanywe kwa siri ili maadui wasijue, kwani huenda wangeweka spana ili Zanzibar iwe dhaifu waweze kuishambulia,” anasema Msekwa.

Spika huyo mstaafu anasema ndani ya siku tano (Aprili 22 – 26) makubaliano yalifikiwa, mabunge yakaridhia, Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakasaini, mambo yakakamilika hadi leo Watanzania wanahesabu siku kutimiza miaka 60.


Alama muhimu za Muungano

Msekwa, ambaye alikuwa Spika wa Bunge kati ya mwaka 1994 – 2005, anasema kwa vizazi vilivyozaliwa ndani ya Muungano (kuanzia mwaka 1965 hadi sasa) vinaona faida zake kuliko mtu mwingine yeyote.

“Nasema hivi kutokana na ukweli kwamba, maisha ya sasa hatuwezi kuyalinganisha na yaliyopita kwa kuwa wengi hawakuwepo, hivyo hawayajui.

“Lakini faida za Muungano, kizazi kipya ndicho wanazifaidi, maendeleo mengi yamepatikana baada ya Muungano,” anasema.

Anasema alama kubwa ya Muungano huu ni upatikanaji wa kutosha wa rasilimali watu, huku akieleza wakati nchi hizo mbili zinaungana mwaka 1964, Tanganyika ilikuwa na watu milioni tisa na Zanzibar ilikuwa na watu 300,000 pekee.

“Hata watu milioni 10 hatukuwa tunafika, tulikuwa wachache ambao kiuchumi hauwezi kuwa mkubwa ukiwa na watu wachache namna hiyo.

“Leo tunafikisha miaka 60, tuko zaidi ya milioni 60, hii ni nguvu ya rasilimali watu, tumekuwa jeshi kubwa, kwa nguvu zetu za pamoja tunakuza uchumi wetu,” anaeleza.

Anasema rasilimali watu inachangia kutengeneza mambo makubwa ya maendeleo kutokana na uwezo uliojengeka katika miaka 60.

“Tunapokwenda kuadhimisha miaka 60, kuna jambo moja tu la kufanya kwa Watanzania, nalo ni kuendelea kuenzi na kuulinda Mungano huu kwa miaka mingine 60, tumuombe Mwenyezi Mungu uzidi kudumu milele na milele,” anasema.


Balaa la Serikali moja, tatu

Katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi wakati wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wananchi wengi walizungumzia muundo wa Muungano.

Wapo waliopendekeza kuwepo kwa Serikali moja, wengine wakitaka Serikali tatu, yaani za Tanganyika, Zanzibar na Muungano.

Hata hivyo, waasisi wa Muungano walipendekeza muundo uliopo sasa wa Serikali mbili; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Msekwa anasema Mwalimu Nyerere alitumia busara Muungano huo uwe na serikali mbili na ndicho kimezidi kuuimarisha hadi sasa.

“Tanganyika ilikuwa ni nchi kubwa, wakati ule tunaungana kama nilivyosema, tulikuwa watu milioni tisa dhidi ya watu 300,000 wa Zanzibar.

“Pia, kijiografia Tanganyika ina eneo kubwa kuliko Zanzibar yenye visiwa vya Unguja na Pemba, tungekuwa na Serikali moja, watu wangechukulia Zanzibar imemezwa na Tanganyika.

Anasema ingeonekana Zanzibar ni ndogo, imekuwa ni mkoa wa Tanganyika, jambo ambalo Nyerere hakutaka kutengeneza sura hiyo.

“Ingekuwa kama ni ukoloni mpya, nchi moja kumeza nyingine, hiyo ni aina mojawapo ya ukoloni. Hivyo, Nyerere hakutaka, akasema lazima Zanzibar ibaki na Serikali yake, ijiamulie mambo yake ili wawepo bila kumezwa na Muungano.

Msekwa anasema kwa mtazamo wake, Serikali mbili ndizo zimefanya Muungano huo udumu hadi sasa unapokwenda kutimiza miaka 60 keshokutwa.

“Hii imetuokoa, kuna nchi nyingine zilizoungana na kuingia kwenye Serikali moja, miungano yao ilivunjiika, mfano ni Misri na Syria, muungano wao ulidumu miaka minne tu, hata kule Afrika Magharibi nchi za Senegal na Ghana, Guinea na Mali au Senegal na Gambia, hazikudumu kwenye Serikali moja.

Anasema kunapokuwa na Serikali moja katika muungano, nchi kubwa ndiyo inakuwa inatawala, inawameza wale wadogo ambao wanakasirika, wanajiondoa na ndicho kingetokea kama Tanzania ingeamua kuwa na Serikali moja.


Hofu ya serikali tatu

Kuhusu muundo wa serikali tatu, Msekwa anasema hilo likifanyika, halafu Tanganyika ikaja kupata Rais mkorofi, nayo italeta shida.

“Tanganyika ina uchumi mkubwa zaidi kuliko Zanzibar na gharama nyingi zinalipwa na upande wa Tanganyika, mfano jeshi ni la Muungano, gharama zake zote zinalipiwa na Serikali ya Muungano ambayo ndiyo hiyohiyo ya Tanganyika.

“Pia, masuala ya mambo ya nchi za nje, mabalozi na uhusiano wa kimataifa yote, haya ni ya Muungano, sasa kama tungekuwa na Serikali ya Tanganyika, akatokea Rais mkorofi akasema tumeungana, hizi ni nchi sawa lazima na gharama tugawane sawasawa, ingekuwaje? Lazima ingeleta matatizo makubwa hata kusababisha Muungano kuvunjika,” anaeleza.

Anasema Mwalimu Nyerere alionyesha busara kusema hakuna kuwameza wadogo (Zanzibar) baada ya makubaliano na kuunda nchi moja watakuwa na kiti kimoja kwenye Umoja wa Mataifa (UN) lakini ndani ya nchi, watu wanaendelea kujitegemea na kuamua mambo yao wenyewe.

“Ndiyo maana leo tunaona Zanzibar inajiamulia yenyewe mambo yake ya maendeleo, elimu, miundombinu na mengine mengi inajiendeleza, nahisi tusingefika miaka 60, kama tungekuwa na Serikali moja au tatu, lakini Serikali mbili ndizo zimetuwezesha kufika miaka 60 bila matatizo, japo kuna kero ndogondogo ambazo zimetatuliwa na nyingine zinaendelea kutatuliwa,” anasema Msekwa.

Msekwa, ambaye ni mzaliwa wa Ukerewe, anasema, zipo kero za Muungano ambazo zimekuwa zikitajwa, ikiwamo za kodi na magari ya Zanzibar yakija Bara yanatozwa ushuru na kuandikishwa upya.

“Kero hizi tumeishi nazo, zinatatuliwa moja baada ya nyingine hadi sasa Watanzania wanakwenda kuadhimisha miaka 60 ambayo kimataifa inaitwa Jubilei ya Dhahabu ambayo Tanzania imeingia kwenye rekodi hiyo ya miaka ya dhahabu