Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moto ulivyoteketeza kituo cha mafuta Geita

Muktasari:

  • Kituo cha mafuta cha Lake Oil kilichopo Geita kimeungua moto unaodaiwa kuanzia kwenye gari lililokuwa likijazwa mafuta

Geita. Kituo cha mafuta cha Lake Oil kilichopo Mtaa wa Mwatulole, Kata ya Bombambili, Manispaa ya Geita, kimeungua moto uliodaiwa kuanzia kwenye gari lililokuwa likijazwa mafuta, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likisema uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, moto huo ulizuka majira ya saa 5:20 asubuhi leo Ijumaa, Julai 10, 2026, wakati gari la mteja lilipokuwa likijazwa mafuta.

Mmoja wa wafanyakazi wa kituo hicho, Ramadhani Guramali amesema gari hilo lilikuwa likijazwa lita 4,000 za mafuta na tayari lita 3,000 zilikuwa zimewekwa kabla ya moto kuzuka.

"Kulikuwa na mteja wetu ambaye huja kuchukua mafuta hapa. Tulikuwa tunamalizia kujaza kontena la mwisho ndipo moto ulipoanzia kwenye betri ya gari, ukasambaa hadi eneo lililokuwa na mafuta na kusababisha uharibifu mkubwa," amesema.

Mfanyakazi wa kituo hicho, Juma Hassan amesema baada ya kugundua moto walitumia vifaa vya kuzimia moto vilivyokuwapo kituoni, lakini walishindwa kuudhibiti kutokana na kusambaa kwa kasi.

"Tulijaribu kuuzima kwa kutumia vifaa vya dharura, lakini ulizidi nguvu na tukalazimika kukimbia. Baadaye gari lililokuwa likijazwa mafuta likateketea na kulipuka," amesema.

Paa la Kituo cha Mafuta cha Lake Oil katika Mtaa wa Mwatulole, Manispaa ya Geita, likiwa limeteketea baada ya moto uliozuka leo, Julai 10, 2026.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Kenneth Mwakasitu amesema kikosi chake kilifika eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto kabla haujasambaa zaidi.

Amesema dalili za awali zinaonesha moto ulianzia kwenye gari lililokuwa likibeba mafuta, lakini amesisitiza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kubaini chanzo halisi.

"Hatuwezi kutoa hitimisho kwa sasa. Tutafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na taasisi husika kabla ya kutoa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha moto," amesema.

Mwakasitu amesema moto huo uliharibu pampu tatu za mafuta, paa la kituo, gari lililokuwa likijazwa mafuta ambalo liliteketea kabisa na gari jingine lililokuwa limeegeshwa ambalo liliungua sehemu.

Gari linalodaiwa kuwa chanzo cha moto uliozuka katika Kituo cha Mafuta cha Lake Oil mkoani Geita likiwa limeteketea baada ya moto unaodaiwa kuanzia kwenye betri kusambaa na kulipua mafuta yaliyokuwa kwenye tenki la gari hilo.

Hata hivyo, amesema jengo la utawala halikuathirika na kikosi cha zimamoto kilifanikiwa kuokoa lita 41,000 za petroli na lita 40,000 za dizeli zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye matenki ya chini ya ardhi, pamoja na magari matatu yaliyokuwa yameegeshwa eneo hilo.

Amesema hakuna mtu aliyefariki dunia wala kujeruhiwa katika tukio hilo.

Kutokana na tukio hilo, Mwakasitu amewataka wanaosafirisha mafuta na waendeshaji wa vituo vya mafuta kuzingatia kikamilifu taratibu za usalama ili kupunguza hatari ya majanga yanayoweza kusababisha hasara kubwa za mali na kuhatarisha maisha ya watu.