Miche ya miti ya Sh100 milioni yagawiwa kwa wananchi

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Godius Kahyarara akikabidhi miche ya miti kwa mkazi wa Kijiji cha Butengo wilayani Chato, Emanuel Maduka miti hiyo imetolewa na shamba la miti Silayo kulia ni Mhifadhi mkuu wa shamba hilo, Juma Mseti
Muktasari:
- Shamba la miti Silayo lililopo wilayani Chato mkoani Geita limetoa miche 250,000 ya aina mbalimbali za miti yenye thamani ya Sh100 milioni kwa wananchi wanaouzunguka shamba hilo ikiwa ni moja ya juhudi za kuimarisha ujirani mwema na kuwajengea wananchi utamaduni wa kupanda miti.
Geita. Wakala wa hifadhi za misitu nchini (TFS) kupitia shamba la miti Silayo umegawa miche 250,000 yenye thamani ya Sh 100milioni kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo ikiwa ni njia moja wapo yakuihamasisha jamii kupanda miti na kupunguza kasi ya ukataji wa miti ya asili.
Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Silayo, Juma Mseti ameyasema hayo leo Desemba 16, wakati wa uzinduzi wa upandaji miti kwenye shamba hilo ulioambatana na ugawaji miche ya miti kwa wananchi na kusema mwamko wa wananchi kupenda kupanda miti umeongezeka tofauti na awali.
Amesema zamani uvamizi wa ulishwaji mifugo eneo la hifadhi pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na mbao ulikua umekithiri, lakini kutokana na elimu ya utunzaji wa mazingira na usimamizi uliopo hali imebadilika na kuwezesha miti iliyopandwa kwenye hekta 4,300.
Amesema lengo la kutoa miche ya miti kwa wananchi ni kuendeleza mazingira mazuri ya ujirani mwema na kuwaonyesha umuhimu wa uhifadhi wa miti ambao unaweza kuwaingizia kipato lakini ni rafiki mzuri wa mazingira.
“Kwa sasa uvamizi umepungua wananchi wanaona faida ya uhifadhi hali ya hewa imebadilika lakini wao pia wanapata fursa ya kulima kwenye maeneo tunayowapa ambayo miti bado ni midogo.
“Hii ya kilimo imekua sio tuu fursa ya chakula, lakini wanalima na kupata mazao ya kuuza na kujiongezea kipato hii imesaidia kuimarisha ulinzi wa shamba maana awali walikuwa wakiingiza mifugo na kuharibu miche sasa hata wao wenyewe ni walinzi wa shamba na tunajivunia kuona wamekuwa sehemu ya shamba hili,” amesema Mseti
Akikabidhi miche hiyo kwa wananchi Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Godius Kahyarara amesema kutokana na mkoa huo kuwa na mifugo mingi, kuna majani ya malisho yamepandwa kwenye eneo la shamba hilo ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Shamba hili ni kubwa lina hekta zaidi ya 69,000 tayari baadhi ya maeneo wamepanda miti na mhifadhi ameniambia bado yapo maeneo tunataka tuwe na uzalishaji wa chakula cha mifugo ili kupunguza ng’ombe kuzagaa na kuharibu mazingira,” amesema Kahyarara.
Aidha kupandwa malisho ya ng’ombe katika eneo hilo kuna faida kubwa na kwamba mbali na kutumika kwa ng’ombe wa Geita pia ni fursa kubwa za kiuchumi.
“Mkoa unamifugo mingi lakini hakuna malisho Kwa kutumia ardhi hii tunaweza kupanda miti na nyasi na kupata malisho pamoja na miti ya matunda na mbao,” amesema Kahyarara.
Hata hivyo, amesema mkoa huo una mkakati wa kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya maisha ya wakazi wa Geita na kuwataka wananchi kuiheshimu kuitunza ili iwe sehemu ya kukuza uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.