Mganga anayedaiwa kuwaambia wavuvi wafanye mapenzi majini adakwa
Muktasari:
- Mganga wa kienyeji amekamatwa jana Jumanne Septemba 3, 2024, akiwa anaendelea na shughuli zake za kuuza dawa hizo kwa wavuvi kwenye fukwe za Ziwa Nyasa.
Nyasa. Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, wamemkamata mganga wa kienyeji maarufu ‘Askofu’ katika Mwalo wa Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa kwa tuhuma za kuwauzia wavuvi wa Ziwa Nyasa dawa za miti shamba akidai zinawaosha nyota na kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) iwapo watashiriki tendo la ndoa ziwani.
Mganga huyo amekamatwa jana Jumanne Septemba 3, 2024, akiwa anaendelea na shughuli zake za kuuza dawa hizo kwa wavuvi kwenye fukwe za Ziwa Nyasa.
Akizungumza na wavuvi hao akiwa ufukweni hapo, Magiri ametoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia kinga wakati wa tendo la ndoa na kuwataka waache kuamini madai ya mganga huyo.
“Kwanza huyu mganga ameingia wilayani kwetu (Nyasa) bila kufuata utaratibu wa kujisajili na hana kibali chochote kutoka kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
"Wavuvi wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Ukimwi ambao unaambukizwa kwa kufanya ngono bila kinga. Hakuna mganga ambaye ana dawa za kutibu au kuzuia ugonjwa wa Ukimwi," amesema Magiri.
Hivyo, amewataka wavuvi kuzingatia maadili na kufanya kazi yao ya uvuvi kwa bidii huku wakiepuka ushawishi kama wa mganga huyo aliouita sawa na utapeli.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Septemba 4, 2024 wakiwa kwenye fukwe hizo, baadhi ya wavuvi wameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua haraka.
Mvuvi Bonface Wadali amesema: “Hata mimi huyu jamaa alikuwa ananikera, nilishamsikiliza siku moja nikasema huyu ni tapeli tu, lakini watu tunauelewa tofauti, wameliwa sana hela na wengine hivi sasa ni wagonjwa.”
Naye Kitara Mbwambwo, anayefanya kazi zake katika mwalo wa Mbambabay ameishukuru timu ya wataalamu wa afya kwa kutoa elimu ya kujikinga na Ukimwi.
“Wavuvi wanarubuniwa sana, wanafanya kazi kubwa na ya hatari na mwisho wa siku wanaambulia magonjwa tu ya zinaa,” amesema Mbwambwo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Steven Mbunda, amesema wilaya hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wote, wakiwamo wavuvi, ili wachukue hatua za kujikinga na maambukizi ya VVU.
Amesema wilaya hiyo ina wakazi 42,338, wakiwamo wanawake 16,443 na wanaume 25,895.
Awali, Mwananchi ilizungumza na baadhi ya wavuvi waliosema hushiriki ngono zembe kwenye maji kwa imani kuwa hawataambukizwa VVU.
Wamesema hufanya hivyo baada ya kuaminishwa na mganga wa kienyeji kwamba kufanya hivyo husaidia kuondoa nuksi na kuongeza mvuto wa kuvua samaki wengi zaidi.
Uchunguzi mdogo uliofanywa na Mwananchi Digital hivi karibuni umebainika kuwa vitendo vya ngono kwenye fukwe za Ziwa Nyasa vimeongezeka baada ya kupewa dawa za mitishamba na mganga huyo.
Inaelezwa dawa hizo zinazoongeza nguvu za kiume na mvuto wa kimapenzi, wavuvi huzinunua kwa Sh5,000 kwa chupa ya nusu lita na hutumia kabla ya kukutana na wanawake.
Wille Mwangono, mmoja wa wavuvi katika ziwa hilo amesema wavuvi wengi wa kiume hufanya ngono bila kutumia kinga, wakiamini huwasaidia kupata mvuto zaidi na samaki wengi.
“Humu kwenye maji ndiyo gesti zetu, tunajifanya tunaogelea kumbe tunafanya mapenzi na hakuna anayegundua,” amesema Mwangono na kuongeza kuwa huwalipa wanawake hao kati ya Sh3,000 hadi 20,000 kulingana na makubaliano.
Zidadu Mbele, amekiri vitendo vya ngono kwenye fukwe za ziwa hilo vimeongezeka, huku akirusha mpira kwa wanaume kwamba huwarubuni wanawake wakafanye vitendo hivyo ndani ya ziwa bila kinga kwa madai si rahisi kupata magonjwa ya ngono.
Hata hivyo, Somoye Hamdani, mkazi wa Mbambabay amesema anaamini wanawake wengi hufanya ngono na wavuvi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Serikali kuwapatia mitaji ili waondokane na biashara ya kujiuza kwa wavuvi.