Mfanyabiashara kortini kwa tuhuma za kujipatia mkopo benki kiudanganyifu

Muktasari:
- Zaidi Bakari anakabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya kughushi nyaraka na kuziwasilisha benki ili kujipatia mkopo wa Sh563milioni kwa njia ya udanganyifu.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Zaidi Bakari, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka 16 likiwemo ya kughushi nyaraka mbalimbali na kuisababishia hasara ya Sh563milioni benki ya NMB.
Bakari amefikishwa mahakamani hapo, leo Oktoba 23, 2023 na kusomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali, Imani Mitume, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo na kuunganishwa na wenzake wawili ambao ni Ernest Omalla na Juma Gululi, ambao walishasomewa mashtaka kama hayo, Oktoba 18, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.
Wakili Mitume amedai kati ya mashtaka hayo 16, mashtaka sita ni ya kughushi nyaraka, mashtaka matano ni kuwasilisha nyaraka za uongo benki, mashtaka matatu ni kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja ni kuisababishia hasara benki ya NMB.
Akimsomewa mashtaka yake, wakili Mitume amedai katika shtaka la kwanza, ambalo ni kughushi nyaraka, Bakari, Omalla na Gululi wanadaiwa kati ya Februari Mosi na Februari 28, 2018 katika jiji la Dar es Salaam kwa nia ya udanganyifu, washtakiwa walitengeneza nyaraka ya ongoa ambayo ni leseni ya biashara yenye namba B 2791473 iliyotolewa Februari 21, 2018 ikionyesha imetolewa na Manispaa ya Ilala, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la pili ni kughushi, ambapo washtakiwa kwa pamoja, wanadaiwa Januari Mosi, 2018 na Januari 23, 2018 maeneo ya tofauti katika jijini Dar es Salaam, walitengeneza leseni ya biashara yenye namba B 2795833 iliyotolewa Januari 23, 2018, ikionyesha kuwa imetolewa na Manispaa ya Ilala, wakati wakijua ni ungo.
Shtaka la tatu, pia ni kughushi ambapo washtakiwa wanadaiwa Aprili Mosi na Aprili 20, 2018, jijini hapa, kwa nia ovu walighushi cheti cha ulipaji kodi safi
kilichotolewa Aprili 20, 2018, kikionyesha kuwa kimetolewa na Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA), wakati wakijua kuwa ni uongo.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Machi Mosi na Machi 13, 2018, Dar es Salaam, kwa nia ovu, walighushi na kutengeneza taarifa ya fedha na kuonyesha kuwa imetolewa na benki ya NBC, wakati wakijua ni uongo.
Shtaka la tano, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Desemba Mosi na Desemba 31, 2018, katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. washtakiwa walitengeneza nyaraka ya uongo ya ukaguzi wa taarifa za fedha zilizoishia Desemba 31, 2017, wakionyesha kuwa imetolewa na benki ya NBC, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Wakili Waziri alidai shtaka la sita pia ni kughushi nyaraka, ambapo kati ya Machi Mosi na Machi 2018 wakiwa katika jiji la Dar es Salaam, kwa pamoja walitengeneza nyaraka ya uongo ya ukaguzi wa taarifa ya fedha iliyoishia Machi 31, 2018, wakionyesha imetolewa na TGA System Associates, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Miongoni mwa mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo kwenda benki, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi Mosi na Desemba 31, 2017, wanadaiwa kuwasilisha nyaraka ya uongo ambayo ni taarifa ya fedha na kuiwasilisha katika benki ya NMB tawi la Kariakoo.
Pia, Machi Mosi na Agosti 30, 2018 kwa udanganyifu, waliwasilisha leseni ya biashara katika benki ya NMB tawi la Kariakoo, wakati wakijua kuwa nyaraka hiyo ni ya kughushi.
Kuhusu shtaka la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi Mosi na Agosti 30, 2018 katika jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kudanganya walijipatia Sh563.35 milioni, kutoka benki ya NMB, tawi la Kariakoo baada ya kuwasilisha taarifa ya uongo ya fedha, wakionyesha imetolewa Machi 3, 2018 na benki ya NBC tawi la Victoria, wakati wakijua ni uongo.
Pia washtakiwa wanadaiwa kuisababishia hasara benki ya NMB, ambapo katika tarehe hizo na kwa nia ovu, washtakiwa waliisababishia benki ya NMB hasara ya Sh563.35 milioni.
Bakari baada ya kusomewa mashtaka yake, alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali.
Hakimu Mrio, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, 2023 kwa ajili ya kusomewa mashtaka na kuhusu mshtakiwa Bakari kupata dhamana, alisema kwa kuwa kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, atatoa masharti ya dhamana yeye.
Kwa upande wake, Omalla na Gululi wao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani hapo na hivyo, wanaendelea kubaki rumande.
Siku hiyo, Hakimu Kabate alitoa masharti ya dhamana ambapo Omalla na Gululi walitakiwa kila mmoja kuwasilisha mahakamani hapo pesa taslimu Sh141.28 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Masharti mengi, washtakiwa hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wenye barua zinazotambulika kisheria, ambapo mmoja kati ya hao wadhamini anatakiwa kusaini dhamana ya maandishi ya Sh141.28 milioni.
Pia wadhamini hao wanatakiwa kutoka ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.