Mchengerwa aagiza kusimamishwa watumishi watano Msalala, Ma-RC, DC

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa.

Muktasari:

  • Serikali imechukua hatua kufuatia malalamiko ya Mbunge wa Msalala, Kassim Iddi Kassim dhidi ya maofisa wa Halmashauri ya Msalala Mkoa wa Shinyanga kuwa wamekuwa wakiwapa adhabu kali watu wakati wa kukusanya kodi.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, ameagiza kusimamishwa kazi watumishi watano wa Halmashauri ya Msalala  Mkoa wa Shinyanga ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kutoa adhabu kali kwa wananchi wakati wa ukusanyaji ushuru.

 Mbali na hilo, Mchengerwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waache kuwatoza wakulima iwapo mazao wanayoyasafirisha yatakuwa chini ya tani moja.

Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo Jumanne Mei 14, 2024 wakati akitekekeza agizo la Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson lililoitaka Serikali kutoa maelezo kuhusu malalamiko ya mbunge wa Msalala, Kassim Iddi Kassim.

Mei 9, 2024, Idd alilalamika bungeni kuwa,  mamlaka za Serikali za mitaa zinatoza ushuru wa mazao shambani kinyume na sheria na wafanyabiashara wasiolipa ushuru huo wanapewa adhabu kali na kupigwa na maofisa wa Halmashauri ya Msalala.

Mchengerwa amesema Mkuu wa Wilaya ya Kahama, alipokea taarifa kuhusu tukio hilo Mei 6, 2024 na kuwa Jeshi la Polisi liliwakamata wahusika wote saa 11.00 jioni jioni.

“Mei 7, 2024 muda wa saa 11.00 jioni wahusika wa tuhuma walitoka mahabusu kwa dhamana,” amesema.

Amewataja wahusika waliokamatwa ni Riston Said, Salehe Hassan, Michael Likomawagi, Francis Mlay, Kassim Rweikiza na kwa sasa, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alimsimamisha mhusika mkuu ambaye alikuwa Dereva wa gari ya ‘task force.’

“Nami nikamshauri awasimamishe wote watano kupisha uchunguzi wa Jeshi la polisi,” amesema Mchengerwa.

Amesema ushuru wa mazao hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, ikiwa mazao ni moja ya vyanzo vya mapato kwa mamlaka za miji, halmashauri za wilaya, mamlaka za miji midogo na halmashauri za vijiji.

Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, ushuru huu unatozwa kwa asilimia tatu ya bei ya kununulia shambani kwa mazao ya chakula na biashara.

“Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, inatamka ushuru huu unalipwa na mnunuzi wa zao alilonunua kutoka kwa mkulima kwa kiwango cha asilimia tatu ya bei ya kununulia shambani,” amesema.

Amesema endapo mfanyabiashara atanunua mazao hayo kutoka shambani kwa mkulima, atapaswa kulipa ushuru huo katika eneo hilo ambalo ununuzi umefanyika.

Mchengerwa amesema ununuzi ukifanyika sokoni ushuru utatozwa katika soko hilo.

Aidha, amesema mazao yanapotoka nje ya halmashauri yanapaswa kuwa yamelipiwa ushuru na endapo itabainika mfanyabiashara anayetoa mazao nje ya halmashauri pasipo kuwa na risiti halali ya malipo ya ushuru, atapaswa kulipa ushuru wa mazao husika na faini.

Amesema mkulima anayesafirisha mazao chini ya tani moja amesamehewa kulipa ushuru huo.

“Ninaomba kutoa rai kwa wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi katika mamlaka za serikali za mitaa kusimamia sheria hiyo kwa kuzingatia masilahi mapana ya pande zote mbili, yaani upande wa mnunuzi na upande wa halmashauri,” amesema.

Amesema halmashauri zinapaswa kukusanya mapato na kutekeleza majukumu mbalimbali yaliyogatuliwa kwao, lakini zifanye hivyo kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesema ni muhimu wafanyabiashara watambue wajibu wao wa kulipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

“Mikoa na wilaya iendelee kutoa elimu juu ya sheria na miongozo mbalimbali juu ya ukusanyaji wa ushuru wa mazao kwa wafanyabiashara waliopo kwenye maeneo yao ili kuwa na uelewa wa pamoja wakati wa utekelezaji,”amesema.

Amesenma Serikali haitovumilia ukiukwaji wa sheria na hatua kali zitachukuliwa kwa watumishi wote watakaokiuka taratibu za kisheria katika ukusanyaji mapato ya Serikali.

Mei 9, 2024, Idd alilamikia bungeni kuwa mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoza ushuru wa mazao shambani kinyume na sheria na wafanyabiashara wasiolipa ushuru huo wanapewa adhabu kali na kupigwa na maofisa wa Halmashauri ya Msalala.

Hatua hiyo ilimfanya Dk Tulia kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo ambalo linasemekana kujitokeza katika halmashauri nyingine pia.