Mbunge aliyefariki ghafla kuzikwa leo Zanzibar

Muktasari:
- Bunge la Tanzania limempoteza Ahmed Yahya Abdulwakil (65), aliyefariki dunia ghafla na mwili wake unatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Buyuni Zanzibar. Ni mbunge wa nane kufariki dunia katika Bunge la 12.
Dodoma. Mwili wa Mbunge wa Kwahani (CCM), Ahmed Yahya Abdulwakil (65) unatarajiwa kuzikwa leo Jumanne, Aprili 9, 2024 kijijini kwao Buyuni Zanzibar.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa jana Jumatatu Aprili 8, 2024 na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kuwa kifo hicho kilichotokana na shinikizo la damu, kilitokea Zanzibar.
“Amefariki ghafla kwa shinikizo la damu. Mazishi ya marehemu yanatarajiwa kufanyika kesho (leo) Aprili 9, 2024 kijijini kwao Buyuni Zanzibar.”
Amesema kwa mujibu wa kanuni za Uendeshaji wa Bunge ya 173 kufuatia msiba huo, leo Jumanne Aprili 9 hakuna kikao cha Bunge ili kutoa fursa ya wabunge kushiriki katika msiba huo.
Abdulwakil alizaliwa Mei 19, 1958. Enzi za uhai wake amekuwa kuwa Mwakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar 2017/2020 na katika uchaguzi mkuu 2020 aligombea uvunge katika Jimbo la Kwahani na kuibuka mshindi.
Jimbo hilo awali lilikuwa linaongozwa na Dk Hussein Mwinyi ambaye mwaka 2020 alipitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais wa Zanzibar na kushinda.
Abdulwakil ni mbunge wa nane kufariki dunia katika Bunge la 12, kati yao watano ni wabunge wa majimbo na wawili wa viti maalumu.
Wabunge wengine waliofariki dunia ni Atashasta Nditiye (Muhambwe), Elias Kwandikwa (Ushetu), William Ole Nasha (Ngorongoro), Said Khatibu Haji (Konde), Martha Umbula na Irene Ndyamukama waliokuwa wabunge wa viti maalumu.
Wabunge wamlilia
Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Muhamed Said Issa ambaye mjumbe mwenzie katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Sanaa na Michezo amesema Abdulwakil alikuwa ni rafiki yake wa karibu licha ya kuwa wanatoka katika vyama tofauti.
“Tukiwa hatuko bungeni huwa ananipigia simu kunisalimia, mara ya mwisho tulikutana naye kwenye boti wiki mbili zilizopita akaniambia mimi ni rafiki yako unaniona siji katika kamati, unashindwa hata kunipigia simu,” amesema.
Amesema kauli hiyo ilimfanya ajisikie vibaya sana na kumfanya kurekebisha makosa yake na nikawa nawasiliana naye.
“Ukweli ni kwamba hakuwa anaumwa na shinikizo la damu, lilikuwa ni suala la mgongo ambalo lilikuwa linamfanya asije bungeni. Sasa hili lililotokea ni suala la siku na wakati umefika, kwa sababu kilichomuondoa duniani ni shinikizo la damu. Kubwa zaidi tumuombee mwenzetu,” amesema.
Naye Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige amesema wameshtuka kwa kifo cha ghafla na kwamba alikuwa muungwana, msemaji na mwenye mchango mkubwa kwenye Bunge.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso ambapo mbunge huyo alikuwa mjumbe kwa zaidi ya miaka miwili, kabla ya kuhamia katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo.
“Mheshimiwa Abdulwakil alikuwa ni mcheshi, mshiriki mkubwa katika mambo ya kibinadamu, kila jambo alikuwa ni lazima ashiriki kwa kweli alikuwa na mchango mkubwa sana, ni huzuni,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Asha Abdallah Juma amesema anamfahamu Abdulwakil tangu akiwa mjasiriamali wa kuuza vyuma kabla ya kugombea ubunge na kuupata.
Amesema mbunge huyo amekuwa na mchango mkubwa katika jamii kwa kujituma kwenye kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali kabla hata ya kuwa mbunge.
“Ameanza kujituma siku nyingi, alikuwa ni mjasiriamali wa kujituma ana mchango mkubwa katika jamii. Mwenzetu kwa kweli ametuachia pengo kubwa hasa katika kipindi ambacho tunamuhitaji,” amesema.