Mbowe awataka wananchi wasidharau siasa, inaamua hatima ya maisha yao

Muktasari:

  • Amesema siasa huathiri bei za bidhaa, kodi, na masuala mengine ya maisha. Godbless Lema aeleza mfumo wa elimu unahitaji kuboreshwa, ili wanafunzi waweze kujiajiri.

Tanga. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amewataka wakazi wa mkoa wa Tanga wasidharau uwepo wa mambo ya siasa na kujiweka pembeni, kwani ndio inaamua hatma ya maisha yao ya kila siku.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai mosi,2024 kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho unaofahamika kama Operesheni +255 uliofanyika maeneo ya Duga.

Amesema bila kujali imani za kichama wala dini, wananchi wanatakiwa kutambua siasa ni maisha.

Amesema wanasiasa ndio wanaamua maisha yao kwamba leo wananchi watakuwa na maisha yapi, ikiwemo suala la kupanga bajeti ambazo wanakutana nazo kwenye bidhaa mbalimbali wanazonunua.

Mbowe ameongeza kuwa siasa ndio inaamua wananchi watalipa kodi kwa namna gani, ikiwemo mambo mengine ya maisha yao, hivyo kwa yeyote atakayeidharau siasa ni lazima akutane nayo kwenye maisha yake.

"Ukiidharau siasa utaikuta kwenye bei ya unga, kwenye nauli na jambo hili linatuhusu Watanzania wote uwe polisi, mwalmu, mkulima na hata uwe mfanyabiashara. Tunatakiwa tuzungumze mustakabali wa nchi hii bila kufumbwa na upovu wa vyama vya siasa, tuulizane elimu wa watoto wetu ni sahihi," amesema Mbowe.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema Serikali inatakiwa kuendelea kuangalia mfumo wake wa elimu ambayo inatolewa kwa watoto wa Tanzania, kwani bado haikidhi katika soko la ajira wanapomaliza.

Anasema mfumo wa elimu unatakiwa endapo mtoto anamaliza elimu yake, aweze kujiajiri na sio elimu ya sasa ambayo mwanafunzi anamaliza shule hana chochote anaweza kufanya anapomaliza masomo.

Pia Lema amezungumzia uwepo wa fursa mbalimbali za kilimo ambazo zinapatikana katika mkoa wa Tanga kama alizeti, machungwa, mbaazi na nyanya, hivyo Serikali iangalie jinsi ya kuwapatia mikopo ya bei nafuu.

Amesema endapo mkulima anapewa mkopo wenye masharti nafuu na kuurejesha wakati anapooanza kuvuna, itakuwa na faida kwao na wataweza kujiendeleza, kwani Tanga ardhi yao ina rutuba ya kutosha.