Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu tofauti zinahitajika kuwainua wanawake

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Girl Effect, Rita Mbeba amesema uwezeshaji wa wanawake ukiwasahau wanaume, hauwezi kufanikiwa kutokana na muundo wa kijamii ambao umempa mwanamume nguvu ya uamuzi.

Akizungumza jijini hapa juzi kuhusu kuwainua wanawake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Rita alisema unaweza kumuelimisha mtoto wa kike na mama, lakini mwisho wa siku, lazima umuelimishe mwanamume ili wote waongee lugha moja.

“Katika jamii zetu wanaume wanatoa maamuzi katika nyanja mbalimbali na hiyo ni tamaduni yetu, hatuwezi kuiacha, kama kuna tamaduni hiyo ni lazima huyo mwenye maamuzi lazima naye kumuelimisha,” alisema Rita.

“Kwa tamaduni zetu, huwezi kumuweka baba nyuma, yeye ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho kwenye mambo mengi, angalia katika familia zetu mama hawezi kufanya vitu fulani bila ruhusu ya mumewe,” alisema.

Alisema ndiyo maana Taasisi ya Girl Effect, pamoja na kufanya kazi sana na wasichana na wanawake, haiwaachi nyuma wavulana na wanaume wakiamini kuwa, ukitaka kumuwezesha mtoto wa kike ni lazima umuhusishe wa kiume, kwa kuwa wanaishi pamoja na maisha yetu ni kusaidiana.

“Kama unavyojua, jamii zetu tunaishi na jinsia zote, hivyo kwa namna yeyote ile hatuwezi kumtenga au kumsahau mwanamume katika harakati zetu,” alisema Rita huku akisisitiza kuwa, mwanamke anayelengwa anaishi na baba, kaka, mjomba, babu na ndugu wengine wa kiume.

Alisisitiza kuwa, kuna changamoto za mwanamke zinahitaji kutatuliwa na mwanamume, hivyo kuwajumuisha wote katika kundi moja, ndiyo njia ya ukombozi.

Rita alisema miongoni mwa mambo yanayofanywa na taasisi anayoiongoza ni kutoa elimu ya afya ya uzazi na katika kufanya hivyo, wanahusishwa vijana wa jinsia zote.

Rita alisema vijana wengi hawafikishi malengo yao na wanaishia katikati kielimu, kwa sababu jamii haitoi nafasi kwa vijana kupata taarifa sahihi.

Alisema hakuna maendeleo kwa mwanamke ambaye hana elimu kubwa, hivyo anaishia kuolewa au kupata mimba akiwa bado mdogo jambo linaloibua changamoto lukuki.

Alisema wasichana wa Kitanzania wapo wanaobakwa, wanaotekelezwa, wengine wanapata uzazi pingamizi, kutengwa na familia kutokana na hali yao huku wengine wakikosa nafasi ya kutoa maoni kama kijana.

"Unakuta kwa sababu mtu amekatisha malengo yake ya kielimu anakuwa na hali ngumu ya kiuchumi. Kwa wale wa kijijini unakosa taarifa ya fursa mbalimbali ikiwamo kujifunza ufundi, elimu ya fedha na mengineyo ya kumuinua kiuchumi,” alisema.

Rita alisema kupitia chapa ya Tujibebe, Girl Effect inatoa jukwaa kwa vijana kupaza sauti, kupata taarifa sahihi na maarifa muhimu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo za kidijitali.

“Madhara makubwa kwa msichana asiyewezeshwa ni mimba za utotoni, unyanyasaji ikiwamo kubakwa na kutengwa na fursa muhimu mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa hawana hata taarifa kuwa akipata mimba anaruhusiwa kurudi shuleni.

Rita alisema jamii inamwangalia mtoto wa kike kwa namna ambayo haimpi kipaumbele kuwa kiongozi hata kama hali inaimarika kidogo, lakini bado safari ni ndefu, kuna wajibu wa kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi mbalimbali katika uongozi.

Ujumbe wake wa Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa juzi, alisema kukiwa na taarifa sahihi, uungwaji mkono, sanjari na kuwa na mazingira rafiki ya kupata haki ya huduma za kijamii na uchumi, wanawake watatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.