Mbegu za asili zaidi ya 1,000 zimeingizwa kwenye mfumo rasmi
Naibu waziri wa kilimo David Silinde (kulia) akizungumza kwenye mkutano wa nne wa kitaifa kuhusu kilimo ikolojia hai Jijini Dodoma leo Machi 3, 2026
Muktasari:
- Wizara ya kilimo imesema hadi sasa inaendeleza jitihada za kutunza mbegu za asili kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kwa kukusanya, kusafisha na kuhifadhi mbegu za asili za mazao 1,000 ambazo zimeingizwa kwenye mfumo kwa ajili ya kutumiwa na wakulima.
Dodoma. Serikali imesema kuwa hadi sasa imefanikiwa kutunza mbegu za asili zaidi ya aina 1,000 ambazo zimeingia kwenye mfumo rasmi ili kuwawezesha wakulima kulima kilimo hai na kutunza mazingira katika mtindo wa ikolojia.
Aidha kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) wizara imefanikiwa kukusanya, kusafisha na kuhifadhi jumla ya mbegu za asili 770 katika mazao ya ulezi, mpunga, mtama, uwele, migomba, maharage na mipapai, wakati Taasisi ya Udhibiti ubora wa Mbegu (TOSCI) imekamilisha utambuzi wa aina 13 za mbegu za asili za mahindi, mpunga na maharage ambazo zimeingizwa kwenye mfumo rasmi wa mbegu.
Taarifa hizo zimetolewa leo Jumanne Machi 3, 2026 na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa nne wa kitaifa kuhusu kilimo ikolojia hai jijini Dodoma uliowakutanisha wadau wa kilimo ili kujadiliana kilimo ikolojia.
Silinde amesema wizara kupitia Tari ina mpango wa kuimarisha upatikanaji wa mbegu za asili na katika mwaka 2025/26 inaendelea kukusanya, kusafisha na kutunza aina 360 ya mbegu za asili za mazao ya mpunga, ufuta, uwele, ulezi, choroko, kunde, migomba, korosho, viazi vitamu, pilipili manga, matango, mbaazi na soya.
“Niwajulishe kuwa, Serikali imedhamiria kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo ili ichangie kupunguza umaskini, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake ili kufikia asilimia 10 ya ukuaji wa kilimo ifikapo mwaka 2030 na katika kutekeleza maazimio ya mkutano wa tatu wa kilimo ikolojia hai uliofanyika mwaka 2023, Serikali imetenga fedha kwenye bajeti ya Wizara ya mwaka 2025/26 ili kuwezesha mkakati wa vyuo kuanza kufundisha kilimo ikolojia ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA),” amesema Silinde.
Amesema Serikali na wadau wa kilimo ikolojia hai bado wanafanya jitihada za kutekeleza kwa ufanisi afua za mkakati ili kufikia malengo ya kilimo endelevu na kuwa na utoshelevu wa chakula kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
Mkurugenzi wa shirika la Kimataifa la SwissAid, Betty Malaki amesema kupitia kilimo ikolojia hai wamewafikia wakulima zaidi ya 8,000 kwa kipindi cha miaka mitano ambapo jumla ya Sh8 bilioni zilitumika katika mradi huo kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mmoja wa wakulima wanaotumia kilimo ikolojia kutoka mkoani Mtwara, Yosefu Kolumba amesema kilimo hicho kimesaidia kuondokana na umaskini kwani kila akilima na uhakika wa kupata mazao tofauti na alivyokuwa analima kilimo cha kawaida.