Mbaroni akidaiwa kummwagia mpenzi wake maji ya moto

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumzia tukio la mwanamke kummwagia mpenzi wake maji ya moto baada ya kumtuhumu kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Inadaiwa Januari 25,2023, Saa 12 jioni, Rehema Prosper (41) alimmwagia mpenzi wake, Timothy Samwel (33) maji ya moto mgongoni baada ya kumtuhumu kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Bujingwa wilayani Ilemela mkoani hapa, Rehema Prosper (41) kwa kosa la kummwagia mpenzi wake maji ya moto mgongoni akimtuhumu kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine.

 Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ameieleza Mwananchi Digital leo kuwa Rehema anadaiwa kutekeleza ukatili huo kwa mpenzi wake, Timothy Samwel (33), Januari 25,2023 Saa 12 jioni.

Mutafungwa amesema; "Huyu aliyefanya tukio hilo alikuwa amefika kumtembelea mpenzi wake kama ambavyo huwa anafanya mara kwa mara lakini baada ya kumfanyia upekuzi kwenye simu yake ya mkononi aliona mawasiliano mbalimbali na wanawake wengine ambao alikuwa aliwatuhumu kuwa wanatoka kimapenzi na mpenzi wake,"

Kamanda Mutafungwa amesema baada ya kubaini uwepo wa mawasiliano hayo, Rehema aliamua kuchukua maji yaliyokuwa yanachemka jikoni kisha kummwagia mwanaume huyo mgongoni jambo lililomsababishia majeraha mwilini huku akisema mwanaume huyo anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Buzuruga  wilayani Ilemela humo.

Kamanda huyo pia amesema Maofisa kutoka dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto mkoani humo wamewasili katika kituo hicho kuchukua maelezo ya mwathiriwa huyo kabla ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanamke huyo.

"Nitoe wito kwa wananchi kujiepusha na matukio ya kujichukulia sheria mkononi, mnapopata hasira mnapokasirishwa na wapenzi wenu siyo jambo jema kuchukua hatua zinazoweza kuleta madhara, huyu dada tutamfikisha mahakamani tukikamilisha uchunguzi wetu," amesema

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital kwa taarifa zaidi....