Mbarawa awashukia uhamiaji wasiotaka ukaguzi

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAA Mussa Mbura akielezea nembo mpya ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam leo Februari 3, 2023.

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amekemea tabia ya maofisa wa Idara ya Uhamiaji Tanzania kukataa kukaguliwa akisisitiza hawana mamlaka ya kukataa ukaguzi wanapotumia viwanja vya ndege vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amepiga marufuku tabia ya maofisa wa Idara ya Uhamiaji Tanzania kupita bila kukaguliwa kwenye viwanja vya ndege, akisisitiza kwamba hawana mamlaka hayo.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Februari 3, 2023 wakati akizindua nembo mpya ya Mamlaka ya Viwanda vya Ndege Tanzania (TAA).

"Mimi Waziri ambaye nimepewa mamlaka ya kusimamia taasisi hii nikiingia lazima nikaguliwe, kwa nini wewe mtu mkubwa au mdogo unakataa kukaguliwa?" amesema Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesema alipata taarifa kwamba kuna vijana waligoma kukaguliwa, huku akimwambia Kamanda wa Uhamiaji wa viwanja vya ndege kuongea na watendaji wake kufuata utaratibu.

"Mimi waziri sijatolewa kwenye utaratibu wa kukaguliwa hata nilipoingia leo nimekaguliwa, kama Viongozi lazima tuonyeshe mfano," amesisitiza Mbarawa.

Kuhusu nembo ya TAA, Profesa Mbarawa ameitaka mamlaka hiyo kuhakikisha inafanya kazi kwa ubora kulingana na kuendana na upya wa nembo hiyo.

Akizungumzia nembo ya TAA, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Dk Ally Possi amesema upya wake ukawe dira mpya ya kiutendaji TAA.

"Viwanja vya ndege vinatoa huduma lakini vinafanya biashara, ubora wa nembo ukaakisi kwenye utendaji wenu," amesema.

Mbali na uzinduzi wa nembo ya TAA Profesa Mbarawa amekabidhi magari manne ya wagonjwa kwa mamlaka hiyo pamoja na kuzindua jengo la watu mashuhuri kwenye kiwanja hicho.