Marekani yatenga dola 1.2 milioni kuboresha afya Zanzibar

Muktasari:
Balozi wa Marekani nchini, Dk Donald Wright amesema wametenga zaidi ya dola 1.2 milioni (zaidi ya Sh2.78 bilioni) kusaidia jitihada za Wizara ya Afya Zanzibar kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Unguja. Balozi wa Marekani nchini, Dk Donald Wright amesema wametenga zaidi ya dola 1.2 milioni (zaidi ya Sh2.78 bilioni) kusaidia jitihada za Wizara ya Afya Zanzibar kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Fedha hizo, Dk Wright amesema zitatolewa na Shirika la Misaada ya Kimataifa (USAID) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani (CDC). Balozi ametoa kauli hiyo baada ya kuzindua kituo kipya cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar, kilichopo Lumumba Mjini Unguja.
Amesema fedha hizo ni sehemu ya uwekezaji muhimu katika sekta ya afya huku akiahidi kwamba Marekani ipo bega kwa bega na Zanzibar katika mapambano dhidi ya corona.
"Kituo hiki ni nyenzo muhimu katika ufuatiliaji maradhi kwa wananchi wa Zanzibar, matumaini yetu ni kwamba kazi zitaongezeka zaidi hasa kutokana na kuwapo kwa janga la corona duniani,” amesema.
Ameahidi kwamba Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha afya za wananchi.
Balozi ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya malaria na Marekani itaendeleza mkakati utakaohakikisha maradhi hayo yanamalizika kabisa.
Dk Wright ameahidi kuwa nchi hiyo ipo tayari kusaidia masuala ya chanjo ya corona ili Zanzibar iendelee kuwa salama na maradhi hayo ambayo yamekuwa tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui amemueleza Balozi Donald kuwa malaria yapo kwa asilimia moja na Wizara ya Afya huchukua hatua za dharura kunapokuwa na mgonjwa mahali popote.
Akizungumzia corona, Waziri Mazurui amesema kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa Zanzibar hajapata mgonjwa wa maradhi hayo na tahadhari kubwa inaendelea kuchukuliwa kwa wenyeji na wageni wanaoingia.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Zanzibar haijaweka vizuizi kwa watu kuingia na kutoka lakini milango mikuu yote ya kuingilia kumewekwa mashine maalumu za uchunguzi kuhakikisha maradhi hayo hayaingia nchini.