Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamia ya wakulima Muheza wanufaika na miche 75,000

Zoezi la upandaji wa miti linalofanywa na Umoja wa Wakulima wa Uhifadhi wa Mazingira UWAMAKIZI katika wilaya ya Muheza  ikiwa ni jitihada za kitunza mazingira katika maeneo yao ambayo ndio chanzo kikuu cha maji yanayopatikana  katika wilaya ya Muheza, Korogwe,Tanga, Mkinga na Pangani. Picha na Mbonea Herman

Muktasari:

  • Upandaji wa miti Muheza walenga kulinda vyanzo vya maji vinavyohudumia Tanga, Mkinga na Muheza huku ukiinua uchumi wa wananchi.

Tanga. Zaidi ya miche 75,000 ya miti ya uhifadhi na mazao ya biashara imegawiwa na kupandwa katika vijiji vya Shembekeza na Kwemwewe, wilayani Muheza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda vyanzo vya maji vya Milima ya Amani na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji katika Jiji la Tanga na wilaya za Muheza, Mkinga, Pangani na Korogwe.

Mpango huo unalenga kukabiliana na uharibifu wa uoto wa asili unaotishia vyanzo vya maji vinavyotegemewa na maelfu ya wananchi.

Miche iliyogawiwa ni pamoja na kakao zaidi ya 24,000, pilipili manga 12,000, karafuu 16,000, mdalasini 9,100, miti ya uhifadhi aina ya kuvukuvu 8,000 na miti ya mbao aina ya sederea 6,000, ikiwa na lengo la kurejesha uoto wa asili na kuongeza kipato kwa wakulima.

Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wa Green Smart City SASA na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Uwasa), kama sehemu ya kulinda vyanzo vya Mto Zigi.

Mwenyekiti wa Uwamakizi, Twaha Mbaruku, amesema juhudi hizo zina lengo la kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.

“Tunapanda miti kwa ajili ya mazingira na uchumi wa wananchi. Bila miti hakuna maji ya uhakika,” amesema.

Aliwahimiza wakulima kuitunza miche ili iweze kukua na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.

Kwa upande wa wanufaika, Mama Hassani alisema mpango huo umeleta mabadiliko chanya, akieleza kuwa tayari ameanza kunufaika kiuchumi kupitia miche ya kakao aliyopata awali.

Mratibu wa Mazingira wa Tanga Uwasa, Ramadhan Nyambuka, alisema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na unaonesha mafanikio ya mradi huo, akibainisha kuwa unalenga pia kuongeza kipato cha wakulima kupitia mazao yanayostahimili hali ya eneo hilo.

Alisisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira ni msingi wa upatikanaji wa maji safi.

“Uoto wa asili ukiharibika, hata huduma ya maji huathirika,” amesema.