Prime
Mambo sita yanayotesa wanafunzi vyuoni

Dodoma. Uraibu wa kamari na mitandao ya kijamii ni miongoni mwa changamoto sita zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu.
Changamoto nyingine ni ya wizi wa mithani, mahusiano ya kimapenzi yanayowasababishia baadhi yao kujaribu kujiua, mapenzi ya jinsia moja na sonona.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu Tanzania (TACOGA 1984), Augustine Matem, baada ya ufunguzi wa mkutano wa 41 wa chama hicho.
Alisema kutokana na changamoto hizo, baadhi ya wanafunzi wamejikuta wakitumia ada walizopewa kwenda kulipia vyuo katika matumizi yasiyolengwa.
Matem alisema wanafunzi wanapaswa kuitumia mitandao kwa mambo ya msingi, lakini wanapoitumia vibaya inawaweka wengi wao kwenye hatari.
Matem alisema wanafunzi hao wanakumbana pia na changamoto ya matumizi mabaya ya muda wawapo chuoni, hali inayowafanya washindwe kusoma na hivyo kujikuta wakifanya wizi wa mitihani.
“Jambo jingine ni uhusiano wa kimapenzi, nafikiri tumesikia matukio mengi kwa vijana wetu ya kujaribu kujiua na wengine kujiua kabisa huku vyuoni, hiyo ni kutokana na wivu wa mapenzi,” alisema.
Alisema wanafunzi wanapofika vyuoni wakiwa na tabia walizozipata katika jamii ni vigumu kuwabadilisha, kwa kuwa wanakuwa wameshakomaa na hivyo wanachofanya ni kuwapa maelekezo ili wajitambue.
Kamishna wa Afya na Mazingira wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahiliso), Christian Kimaro alisema kumekuwa na matukio mengi yanayosababishwa na afya ya akili, lakini yanafananishwa na utovu wa nidhamu.
Alisema matatizo ya afya ya akili yanasababishwa na kubadilisha mazingira, kuishi nje ya vyuo baada ya kukosa hosteli za vyuo, uhuru wanaoupata vyuoni na utamaduni usio mzuri unaowafanya wengine kuiga.
Sababu nyingine ni ugumu wa maisha unaoanzia kwenye familia, huwafanya wanafunzi washindwe kujisimamia wawapo vyuoni.
“Alisema katika tathimini iliyofanywa katika moja ya vyuo nchini, iligundua asilimia 41.4 ya wanafunzi wamepata sonona na kati ya hao, asilimia 11 wamepata mawazo ya kutaka kujidhuru ama kujiua.
Awali, akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Franlin Rwezimula aliomba washauri hao kuwasaidia wanafunzi kujiajiri kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoupata darasani.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Razak Lokina alisema jukumu la ulezi halijawahi kuwa rahisi katika kipindi hiki kwa kizazi kilichopo, tofauti na wakati wakisoma ambapo walikuwa wachache na hakukuwa na mitandao ya kijamii.
Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wanafunzi kuzuiliwa matokeo yao kwa kutolipa ada za masomo kwenye baadhi ya vyuo.