Mama lishe kariakoo wapata ahueni baadhi ya maduka kufunguliwa

Muktasari:

  • Mama lishe wa Kariakoo waeleza ahueni yao siku ya leo baada ya baadhi ya maduka kufunguliwa, ingawa wanasema wanasikiliza kinachoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja.

Dar es Salaam. Baadhi ya kina mama lishe wanaofanya shughuli zao katika soko la Kariakoo wamesema hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kufungua maduka yao ni kama neema imeanza kuonekana kwao.

Hayo wameyasema leo Jumatano Mei 17, 2023 wakizungumza na Mwananchi huku wakilalamika juzi na jana mazingira ya biashara hayakuwa mazuri kwao kutokana na watu wachache kuwepo Kariakoo, kwa sababu baadhi ya maduka yalikuwa yamefungwa kutokana na mgomo.

Kuhusu mwenendo wa shughuli zao baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuweka msimamo wa kutofungua biashara licha ya kuahidiwa kutatuliwa changamoto zao Fatuma Abdallah amesema anatamani mgomo umalizike kwasababu maisha yake yanategemea kazi hiyo ambayo wateja wakuu ni wafanyabiashara wa soko hilo.

"Siku hizi mbili zimekuwa ngumu sana kwetu ukiangalia wengine tuna mikopo ukija huku na kukosa kipato ulichozoea inabidi kuumiza kichwa ili kupata ulichopungukiwa.

"Niliposikia leo kuna mkutano niliamua kuongeza kipimo cha vyakula kama zamani lakini nimesikia muda huu bado mkutano haujaanza, ingawa hali ya wateja sio mbaya tofauti na siku zilizopita,"amesema Fatuma.

Naye, Irene Raphael anayeuza chakula wakati wa mchana sokoni hapo amesema amejikuta anatumia hadi mtaji wake kutokana na baadhi ya wafanyabiashara ya wateja kumkopa chakula kwa sababu ya shughuli kutofanyika kwa ufanisi katika eneo hilo.