Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama anayekamua lita 40 za maziwa yake mwenyewe

Mama anayekamua lita 40 za maziwa yake mwenyewe

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya wanawake wakiogopa kuwanyonyesha watoto wao kwa madai kuwa wataharibu muonekano wa matiti, hali ni tofauti kwa wakili Anastazia Muro (33), aliyeweka nadhiri ya kunyonyesha watoto wake kwa miezi sita bila kuwapa chochote huku akiwa ameanza kukamua maziwa na kuweka kwenye pakiti.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wanawake wakiogopa kuwanyonyesha watoto wao kwa madai kuwa wataharibu muonekano wa matiti, hali ni tofauti kwa wakili Anastazia Muro (33), aliyeweka nadhiri ya kunyonyesha watoto wake kwa miezi sita bila kuwapa chochote huku akiwa ameanza kukamua maziwa na kuweka kwenye pakiti.

Tangu anaanze kukamua maziwa yake miezi miwili iliyopita ameshahifadhi pakiti 200 za maziwa zenye ujazo wa mililita 100 ambayo ni sawa na lita 40 au ndoo kubwa mbili za maji.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, maziwa ya mama pekee ni chakula na kinywaji tosha kwa mtoto mchanga kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha yake.

Anastazia, ambaye ni Meneja Programu katika Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), mtoto wake wa kwanza, Raphana ametimiza miezi mitatu.

Anasema aliamua kukamua maziwa na kuyaweka kwenye pakiti, baada ya kujifunza kutoka katika mitandao ya kijamii wakati akijiandaa kumpokea mtoto wake.

“Nilipopata ujauzito nilianza kuingia mitandaoni kusoma taarifa mbalimbali. Nilitaka mwanangu anyonye maziwa yangu pekee,” anasimulia Anastazia.

Pia, anasema alijifunza mengi akaanza kuandaa maziwa kwa kula vyakula vinavyotakiwa akiwa na ujauzito wa miezi saba.

“Nilianza kula unga wa mbegu za maboga na vyote vinavyoelekezwa, nikaandaa vifaa vya kukamulia na namna nitakavyohifadhi.”

Anastazia anasema baada ya kujifungua alipata changamoto kwa kuwa alipata mtoto kwa njia ya upasuaji, hivyo maziwa hayo kuanza kutoka mapema.

Hata yalipoanza kutoka hakuanza kukamua muda huohuo kutokana na changamoto nyingi zilitokea, ikiwamo chuchu kuchubuka, hivyo alianza rasmi baada ya mtoto kutimiza umri wa siku 40.

“Kuna tofauti anavyonyonya na kukamua, kabla ya kuanza kukamua yalikuwa mengi yanamzidi mtoto, lakini siku ya kwanza nakamua yalitoka kidogo kama mililita 60, lakini siku ya pili nikafikisha mililita 100 yakaendelea kuongezeka,” anasema Anastazia.

Anastazia, ambaye ameshamaliza likizo ya miezi mitatu ya kujifungua, anatarajia kuanza kazi kesho na tayari ameanza kumfundisha mwanawe kunywa maziwa kupitia chupa ili azoee mapema kabla hajaanza kuwa mbali naye.

Kupitia baraka hiyo, Anastazia anafikiria ni namna gani ataweza kuhudumia watoto wenye uhitaji.

“Nina uwezo wa kutoa maziwa ya kumtosha mtoto na kuyahifadhi, ninatoa maziwa ambayo mwanangu hawezi kuyamaliza ndiyo maana ana afya nzuri licha ya kwamba ninayakamua.

“Kwa jinsi nilivyoangalia nchi za wenzetu watu wanatoa msaada wa haya maziwa kwa wenye uhitaji, mpaka sasa nimeongea na watu tofauti, ninafuatilia jinsi ambavyo ninaweza kuwasaidia wale wenye uhitaji.”

Anasema kwa sasa anaangalia namna miongozo inavyotaka, lakini kama ni Serikali au mtu binafsi anaweza kutoa msaada huo.

“Nipo tayari kutoa msaada kwa wazazi ambao wamepata matatizo au changamoto baada ya kujifungua, wapo yatima pia,” anasema.

Hata hivyo, Anastazia anasema mbali na mafanikio hayo, asilimia 50 imechangiwa na mumewe, Raphael Mgaya ambaye anamsaidia katika mambo mengi, ikiwemo kuhakikisha hapati msongo wa mawazo.

“Mchango wa mume wangu ni mkubwa, yeye ndiyo baba wa familia, anahakikisha ninakula vizuri, hanipi msongo wa mawazo, ananisaidia kupumzika, usiku atambeba mtoto ataniambia lala pumzika, atanitia moyo katika kunyonyesha,” anasimulia Anastazia.

“Ataniuliza vitu gani ninataka, ana mchango mkubwa, naweza sema asilimia 50 amezichangia mimi kutoa maziwa yote haya.”


Anakula nini?

Anastazia anasema licha ya homoni kuwa chanzo cha uzalishaji maziwa, anakula vyakula kwa mpangilio na mlo kamili, ikiwamo dagaa, nyama na samaki.

Anasema vyakula hivyo, mara nyingi hupenda kuchanganya mbegu za maboga kwa kuwa zina zink ya kutosha inayosaidia uzalishaji wa maziwa, uwatu na pilipili manga.

“Nikiamka natengeneza mchangamnyiko wa mbegu za maboga, uwatu, pilipili manga nikichanganya na maji ya moto ya tangawizi unakuwa kama uji, saa nne nakunywa supu ya samaki au kuku, chakula cha kawaida mchana kwa kuzingatia makundi matano ya chakula bila kusahau matunda nanasi au papai na jioni uji kama wa asubuhi, kisha usiku chakula na matunda tena,” alisema.

Jinsi ya kuandaa maziwa

Anastazia anasema maziwa yaliyogandishwa yana utaratibu maalumu wa kuandaliwa kabla mtoto hajapewa.

“Yakitaka kutumika yatawekwa kwenye bakuli au kikombe hayatakiwi kuchemshwa, yakiyeyuka yatawekwa kwenye chupa yake na mtoto akitaka kunywa yatawekwa kwenye bakuli yenye maji moto ili yapate uvuguvugu unaofanana na maziwa ya mama na kisha mtoto atayanywa,” anafafanua.