Mama adaiwa chanzo mikono ya mwanae kukatwa
Muktasari:
Atuhumiwa kuchoma moto vidole vya mtoto huyo na kumfungia ndani bila matibabu
Shinyanga. Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mwanono, Kata ya Didia Mkoa wa Shinyanga anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumchoma moto mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 14, kwenye vidole vya mikono hali iliyosababisha majeraha makubwa, kuoza kisha mikono kukatwa.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika kijiji hicho baada ya mtoto huyo kutuhumiwa na mtu mmoja kuiba simu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema jana kuwa mzazi alifikia uamuzi wa kufanya ukatili huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mtu aliyeibiwa.
Kamanda Kamugisha alimnukuu mama huyo, akisema alitoa adhabu hiyo kwa kuwa mwanaye alikuwa tabia ya wizi.
“Mama huyo alimchukua mtoto na kumfunga majani na mifuko ya plastiki mikononi, kisha akamchoma moto katika vidole vyake vya mikono miwili,” alisema Kamanda Kamugisha.
Alisema baada ya hapo mama huyo alimfungia ndani ya nyumba mtoto huyo bila kumpatia matibabu yeyote.
“Kutokana na hali hiyo mikono ya mtoto huyo iliyokuwa na majeraha ilioza... baada ya kugundua hivyo, mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kupatiwa matibabu ya upasuaji kwa kukatwa mikono,” alisema Kamanda Kamugisha.
Alisema mtoto huyo amelazwa katika hospitali hiyo huku akiendelea na matibabu na hali yake ni mbaya.