Malecela: Tumuenzi Magufuli kwa kukamilisha miradi aliyoianzisha
Muktasari:
- Wakati Watanzania wakiendelea na maombolezo ya siku 21 za kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela amesema njia nzuri ya kumuenzi ni kukamilisha miradi yote aliyoianzisha.
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiendelea na maombolezo ya siku 21 za kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela amesema njia nzuri ya kumuenzi ni kukamilisha miradi yote aliyoianzisha.
Malecela alieleza hayo wakati akihojiwa na televisheni ya Azam kuhusu kifo cha Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Malecela amesema hata bila maono kama watendaji waliosalia watatekeleza miradi aliyoianzisha kama reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, kuliimarisha Jiji la Dodoma na ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme kitakuwa kitu kizuri.
“Hata bila ya maono kama tutatekeleza yale yote aliyoyaanzisha na kufikisha kule alikokuwa anategemea litakuwa jambo la kumuenzi Magufuli na kumshukuru Mungu,” amesema Malecela.
Waziri mkuu huyo mstaafu amesema ana imani na Rais mpya, Samia Suluhu Hassan kwamba kama amefanya kazi na Magufuli ni wazi kuwa ana uwezo mkubwa kiutendaji.
“Namtakia mafanikio mema Samia Suluhu na mpaka sasa ameonyesha uwezo mkubwa kama aliweza kufanya kazi kwa kasi ya Magufuli atakuwa kiongozi bora, lakini pia kama watanzania tutakuwa tunatekeleza wazo kwamba hatujali jinsia ila tunaangalia utendaji wake kwa Taifa,” amesema Malecela.
Amewataka Watanzania kusikitika kwa kuwa kifo cha Magufuli ni mipango ya Mungu.