Malecela aisifia miradi ya Magufuli, ampongeza Samia kuiendeleza

Waziri Mkuu mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Malecela akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma
Muktasari:
- Waziri Mkuu mstaafu John Malecela amezungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi inayotekelezwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kile alichokiacha mtangulizi wake, John Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17, 2021.
Dodoma. Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara, John Malecela ameshukuru miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoiendeleza.
Malecela ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu wa saba wa Tanzania ameyasema hayo leo Jumapili Juni 25, 2023 nyumbani kwake Kilimani, Dodoma alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Samia aliyekuwa makamu wa Rais kuanzia Novemba 5, 2015 baada ya uchaguzi mkuu huku Rais akiwa John Magufuli, aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021 baada ya Magufuli kufariki dunia Machi 17.
Malecela amewataka Watanzania kumpa nafasi Rais Samia ambaye anafanya kazi usiku na mchana katika kuliletea maendeleo Taifa hili.
“Kwa mfano, katika Tanzania baada ya miezi 12, tukifika mpaka mwaka kesho reli ya SGR au reli ya mwendokasi itakapokuwa tayari, Watanzania tutakuwa katika dunia mpya, dunia ambayo unatoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa saa tatu, saa moja na nusu Morogoro, saa moja na nusu Dodoma kwa treni ya mwendokosi.
“Na nadhani tutakuwa katika nchi chache za Bara la Afrika zenye aina hiyo ya usafiri. Sasa hii italeta maana gani, italeta maana kwamba wenzetu wa Rwanda, Burundi, Congo nao watafaidika, kwa sababu mizigo yao kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma itachukua muda mfupi zaidi,” amesema.
Malecela amewahi kushika nyadhifa mbalimbali tangu Serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, amesema uendelezaji wa miradi wa Bwawa la Nyerere utaiwezesha nchi kufanya biashara ya umeme nje ya nchi.
“Umeme utakaotoka hapo utaifanya Tanzania iwe mbaali. Ni juzi tu nilikuwa naangalia TV naona Afrika Kusini sehemu za miji yao hazina umeme. Lakini, sisi Tanzania tutakapofika mwaka kesho tutakuwa na umeme wa kutosha na kuanza kufanya biashara ya umeme kuwauzia majirani zetu ambao hawana umeme wa kutosha,” amesema.
Pia, amempongeza Rais Samia kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi mkoani Mwanza litakalokuwa la sita kwa ukubwa Afrika lenye upana wa mita 28.4 na urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.65 litakalogharimu Sh700 bilioni.
“Napenda nichukue nafasi nimtakie marehemu aliyekuwa Rais wetu wa awamu ya tano (John Magufuli) nimtakie makazi mema huko aliko, kwamba nimtakie kila la kheri, Mungu ambariki amuongezee thawabu zote anazoweza.
“Kwa sababu Magufuli alituachia vitu vya maana sana na kimoja wapo ambacho mimi nina hakika hatukukifiria Tanzania tungeweza kupata kitu cha namna ile ni cha kujenga reli, kujenga barabara, kujenga daraja ka Busisi.
“Na Mama (Rais Samia) pia amelikazania kwamba liweze kumalizika mapema zaidi,” amesema.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi siyo tu kutaondoa adha ya kusubiri na kutumia vivuko, bali pia kutapunguza muda wa kuvuka eneo hilo kutoka wastani wa dakika 40 hadi saa mbili hadi kufikia dakika nne.
Daraja hilo litaunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema za mkoani Mwanza pamoja na mikoa ya Mwanza na Geita.
Mradi huo utakapokamilika utaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) litakuwa na urefu wa Kilomita 3.2 likipita juu ya Ziwa Victoria.
Pia, utahusisha ujenzi wa barabara unganishi wenye urefu wa kilomita 1.6 na fedha zote za utekelezaji zinatokana na mapato ya ndani.
Daraja hilo ni la sita Afrika likitanguliwa na la Misri likiwa na urefu wa kilomita 20.5, ikifuatiwa na lililoko nchini Nigeria lenye urefu wa kilomita 11.
Madaraja mengine marefu na kilomita zake kwenye mabano ni Suecanal lenye kilomita 3.9 na mengine mawili yiliyoko nchini Msumbiji yenye urefu wa kilomita 3.8 na 3.6.
Miradi hiyo pamoja na daraja la Kigongo Busisi inatekelezwa na Rais Samia aliyeapishwa kushika uongozi wan chi Machi 19, 2021 akichukua nafasi ya Rais Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Akizungumza baada ya kuapa kuchuku uongozi wan chi Rais Samia alisema:
“Dk Magufuli alikuwa kiongozi asiyechoka kufundisha, amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mpenda maendeleo na mwanamapinduzi ya kweli.”