Makomandoo ‘siyo watu wa kawaida’

Komando wa jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kionyesha ujasiri wa kulalia misumari huku mwenzake akiwa amemkanyaga kifuani wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Picha na Anthony Siame
Muktasari:
- Ujasiri, ukakamavu na ugumu wa miili yao ni baadhi ya vitu vilivyowashangaza watazamaji ambao wamekuwa wakisikia sifa nyingi za makomando, lakini bila kujua uwezo walionao tofauti na wengine.
Dar es Salaam. Kikosi cha makomando cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kimekonga mioyo ya watazamaji waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika, zilizofanyika jijini Dar es Salaam.
Ujasiri, ukakamavu na ugumu wa miili yao ni baadhi ya vitu vilivyowashangaza watazamaji ambao wamekuwa wakisikia sifa nyingi za makomando, lakini bila kujua uwezo walionao tofauti na wengine.
Kikosi hicho cha makomando 21 kikiongozwa na Luteni Mrope, kiliingia uwanjani na kuonyesha mbinu mbalimbali za kupambana na adui bila kutumia silaha na kuufanya Uwanja wa Uhuru ulipuke kwa shangwe muda wote wa maonyesho hayo.
“Hawa jamaa siyo watu wa kawaida. Binadamu wa kawaida hapo anapoteza maisha,” amesema Said Mzee.
Makomando hao walianza kupigana kwa mbao mpaka zinavunjika na kulifanya jukwaa kuu lililokaliwa na viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais John Magufuli, kuangua vicheko hasa baada ya komandoo mmoja kupigwa kwa ubao kwenye ugoko hadi ukavunjika.