Majeruhi 20 wa ajali Kiteto watajwa

Baadhi ya majeruhi wa ajali ya basi dogo lililoanguka Kijiji cha Chekanao Wilayani Kiteto mkoani Manyara, wakisafirishwa kuelekea Hospitali ya Rufaa Jijini Dodoma. Picha na Mohamed Hamad
Muktasari:
- Majina ya waliofariki kwa ajali ya basi Kijiji cha Chekanao Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, yametajwa sambamba na waliolazwa Hospitali ya Kiteto na waliosafirishwa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi hali zao zaanza kuimarika.
Kiteto. Hali za majeruhi 20 wa ajali ya basi dogo lililoanguka Kijiji cha Chekanao Wilayani Kiteto mkoani Manyara, imeimarika baada ya kupewa matibabu.
Majeruhi hao walifikishwa katika kituo cha afya Mrijo Wilayani Chemba, Hospitali ya Wilaya ya Kiteto na wengine wamefikishwa Hospitali ya Rufaa Mkoani Dodoma.
Ajali hiyo ilitokea Septemba 19, 2022 Kijiji cha Chekanao Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, baada ya basi aina ya Mitsubishi lililokuwa likitokea Kijiji cha Matui Wilayani Kiteto kuelekea Wilaya ya Kondoa kuanguka na kusababisha vifo na majeruhi 20.
Akizungumza na Mwananchi, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Kiteto, Dk Erastos Sakweli alimewataja majeruhi hao kuwa ni Hadija Saidi (50), Muhtashiu Juma (24), Iddi Said (8), Sarah Juma (27), Ibrahimu Saidi (5), Madawa Ally (75).
Soma zaidi:Sita wafariki ajali ya gari Kiteto
Wengine ni Halima Ramadhani ((39), Amina Hamisi (34), Kamru Nurdini (4) Mohamed Mikidu (40) ambao kwa pamoja walisafirishwa kwenda matibabu Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
“Hali za majeruhi waliolazwa Hospitali ya Kiteto sio mbaya na wanaendelea na matibabu kufuatia kuumia maeneo tofauti ya miili yao kutokana na ajali ya basi hilo iliyotokea Kijiji cha Chekanao Wilayani Kiteto,” amesema Dk Sakweli.
Alisema katika hospitali ya Wilaya ya Kiteto amepokea mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Mbuse (65) ambaye alipoteza maisha akisafirishwa kuelekea Hospitali ya Kiteto kutokana na ajali hiyo huku kukiwa na majeruhi 20.
Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi akizungumzia ajali hiyo alisema watu wanane wakiwemo wanawake wanne na wanaume wanne walipoteza maisha kutokana na ajali hiyo.
Waliopoteza maisha ni Farihia Abtwalib (3), Mariamu Ramadhani (48), Zauda Ally (45), Husuna Chobu (1), Jasia Athumani (35), Salumu Hssani (45), Azizi Mohamed (54), na Emmanuel Mbise (65).
Ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi wa gari hilo basi aina ya Mitsubishi ambapo dereva ambaye jina lake halikufahamika mapema alishindwa kumudu gari na kusababisha ajali hiyo.
“Ajali hii kimsingi imetokana na uzembe wa dereva mwenyewe yeye mwenyewe alishindwa kumudu gari kutokana na mwendo kasi na hata abiria wangeweza kupiga kelele ili dereva apunguze mwendo huenda ajali hiyo sisingetokra kizembe,” amesema RPC Katabazi.
Nao baadhi ya abiria ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema basi hilo lilikuwa linafukuzana na basi lingine lililokuwa linasafiri kuelekea Babati huku wao wakienda Kondoa hivyo huku njiani walikuwa wananyanganyana abiria.