Majanga kwa shule zisizo na uzio

Mazingira ya moja kati ya shule zisizo na uzio jijini Dar es Salaam. Picha na Devotha Kihwelo

Dar es Salaam. Ni janga. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na changamoto wanazopita wanafunzi katika shule zisizo na uzio jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, shule hizo zimejikuta zikiwa na muingiliano na wanajami wakiwamo watembea kwa miguu na waendesha bodadoda huku baadhi ya madarasa yakielezwa kutumika tofauti na makusudio hasa nyakati za jioni na usiku.

Changamoto hizo zinaikabili shule za msingi Bangulo, Kinyerezi, Yangeyange, Ukonga Jica na Msongola zilizopo jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika shule hizo umebaini kuwa changamato hizo zimekithiri, hivyo kuleta wasiwasi katika upatikanaji wa elimu bora.

“…wapita njia imekuwa ni sehemu yao ya kujidai na kusahau kuwa ni eneo la shule na wakati mwingine wanapita kwa kupiga kelele.

“Waendesha bodaboda nao wamekuwa wakikatiza eneo la shule, huku wakiwa wamewasha muziki kwa sauti ya juu, jambo linalowakosesha utulivu wanafunzi madarasani,” anasema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msongola Mpya, Mabruki William ambaye shule yake ina wanafunzi zaidi ya 2,900.

 Anasema kuwepo uwanja katika eneo la shule unaotumiwa na wananchi, ni kama chaka la kufanyia maovu kwa sababu si sehemu zote zina taa za kuwafanya waonekana. “Hali hii inatoa mwanya kwa watu hao kufanya kile wanachojisikia.”

Mwalimu William anasema kutokana na eneo lilivyo, imefikia hatua hata vyoo vya shule vinatumiwa na watu wasio wanafunzi wala wafanyakazi wa shule.

Hali hiyo pia anasema inasababisha uwepo wa matukio ya wizi wa mara kwa mara wa mali za shule, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya shule.

“Tumeshaibiwa mashine ya kupandishia maji, koki za mabomba, matukio haya yanatokea hasa mwishoni mwa wiki. Pia watu wanakuja kujisaidia kwenye vyoo vya shule, kitu ambacho si sawa, kwani watu wanaweza kuwa na maradhi yao hivyo ni rahisi kuwaambukiza wanafunzi, wakati mwingine wanaacha vyoo vichafu watoto wanalazimika kusafisha,” anaeleza Mabruki.

 Anasema kwa kuwa madarasa hayana milango, baadhi ya wananchi huyatumia isivyo na wakati mwingine wanasahau nguo zao.

Kwa shule ya Bangulo yenye majengo mapya na mengine chakavu, inaelezwa ina wanafunzi zaidi ya 3,000 huku ikiwa na walimu 16 pekee.

 Shule hiyo ipo eneo lenye kilima, mbaya zaidi hakuna uzio, hivyo wanafunzi kuchangamana na wananchi kwani njia inayotumika kuelekea kwenye makazi ya watu ni ya kukatisha katika eneo la shule.

“Kweli tuna changamoto ya uzio katika shule yetu ambayo inasababisha muingiliano wa jamii inayotuzunguka, hivyo kuwatoa watoto kwenye umakini wakiwa darasani,” anasema mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Bangulo, John Sendeu.

Anasema hali hiyo inatoa mwanya kwa baadhi ya wanafunzi kutoroka wakati wa masomo kwa kuwa hakuna kizuizi chochote.

Alipoulizwa kuhusu makorongo yaliyopo katika shule hiyo, mwalimu huyo alisema mambo mengi yanaweza kujibiwa na Mkurugenzi wa Jiji.

“Mashimo unayoyaona ni hatari lakini siwezi kujibia jambo hilo lipo chini ya Mkurugenzi, hivyo kwa taarifa ya majengo na haya mtafute yeye atakujibu,” anasema Sendeu.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura anasema mambo yote yamejadiliwa yakiwemo ya shule ya Bangulo na tayari wana fedha za ujenzi zikiwamo za ukarabati.


Changamoto kwa wanafunzi

Abdul Hassan, anayesoma Shule ya Msingi Bangulo anasema wanakosa sehemu ya kucheza kwa sababu mazingira yao ni hatari kutokana na mashimo, hivyo wengi wanaogopa kuumia.

“Hapa shuleni kwetu hatuna pa kucheza, wengine wanaumia na mvua ikinyesha maji yanakuwa mengi tunakaa darasani tunaogopa kushuka chini kununua vyakula,” anasema.

Happiness John, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Msongola Mpya anasema wakiwa nje wakati wa masomo wanashindwa kumsikiliza mwalimu kutokana na kelele za bodaboda wanaopita eneo hilo.

“Sisi darasa letu tunasoma nje, mwalimu akiwa anatufundisha tunawaona wenye pikipiki wanapita, tunawashangaa na wakati mwingine wanawasha muziki kwa sauti kubwa,” anasema Happiness.


Wazazi wanena

Peacenesia Josephat, mkazi wa Bangulo anasema miundombinu ya shule si rafiki kwa watoto, hivyo wanapata wakati mgumu wakati wa masomo.

“Kwanza shule ina madarasa machache, watoto wanakaa chini hata eneo la kuchezea hakuna kutokana na makorongo yaliyopo, mwingine nakaa kibarazani kuangalia watoto wanavyopata shida katika michezo.

“Wakikimbizana na bahati mbaya mtoto akiteleza ni rahisi kuvunjika mguu kutokana na mazingira yalivyo hayaridhishi,” anasema Peacenesia.

Pia anasema ili kuzuia utoro kwa wanafunzi, walimu wanalipisha wazazi matofali kwa mwanafunzi aliyebainika kutoroka ili kuendelea kuboresha miundombinu ya shule.

“Kwa sasa wala hamfukuzi mtoto shule, wanachokifanya mzazi unaitwa unasomewa mashtaka ya mtoto na mzazi unapewa adhabu ya kununua matofali kama mawili au tatu ili kuendeleza majengo ya shule,”anasema.

Kwa upande wake, Denis Lazaro anasema wingi wa wanafunzi na uchache wa madarasa hautoi nafasi kwa watoto kusoma na kuandika vizuri kwa sababu ya kukaa chini.

“Kutokana na uchache wa madarasa na madawati, mtoto wangu anakaa chini kila siku na kuumwa mafua kutokana na vumbi la darasani na nguo zake zinachafuka. Pia makorongo yaliyopo shuleni ni hatari kwa usalama wa watoto,” anasema.

Siwatu Abdalah, mkazi wa Msongola anasema watu wanajikuta wanakatiza katika mazingira ya shule kwa kuwa ni njia ya mkato kwenda kituo cha afya kilichopo jirani na shule hiyo.

“Kupita barabarani ni mbali, hatuoni sababu ya kutokatisha katika shule na wakati mwingine hatujui kama wapo darasani tunafikiri wanacheza tunapowaona nje wamekaa,” anasema Siwatu.


Kauli ya Serikali

Ofisa Elimu Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam, Abilah Mchia anasema anatambua changamoto zilizopo katika wilaya hiyo ikiwamo ukosefu wa uzio, makrongo maeneo ya shule, madarasa kutokuwa na milango na mengine ambayo ni hatarishi kwa wanafunzi.

Anasema changamoto hiyo si tu katika shule ya Bangulo bali ipo katika shule ya Jica amabyo pia ina makorongo.

 Anasema ameshaandaa ripoti ya Septemba kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Mkurugenzi kwa hatua ya utekelezaji.

“Kuna shule nyingi bado zina changamoto, hivyo kutokana na bajeti ilivyo tunajitahidi kuwekeza katika kila sehemu ambayo ni muhimu, mkurugenzi atatupa majibu ili kuendeleza pale tulipoishia,” anasema Mchia.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Yangeyange, Mrisho Goha anasema changamoto za shule zilizopo katika mtaa wake ni nyingi na kudai wazazi wanachangia kwa kutofika kwenye vikao pindi vinapoitishwa.

“Sisi tunasema shule ni ya jamii si ya Serikali tena, kwa sababu watoto wanaosoma hapa ni wa kwetu, ukiitisha kikao kueleza changamoto na nini kifanyike wazazi hawajitokezi, lakini wao wanakuwa wa kwanza kulalamika,” anasema Goha.

 Anasema shule za mtaa wake zipo tatu na zote hazina uzio ikiwepo shule ya Msongola Mpya ambayo ina madarasa manane na matundu ya choo 10.

Hivyo, anasema bado kuna uhitaji wa hivyo vitu kutokana na idadi ya wanafunzi shuleni hapo.

“Tunatamani kuzungumza na watu wote ili tuwachangishe, lakini tatizo linalojitokeza si wote ni wakazi wa huku, pia kuna watu watoto wao wanasoma shule binafsi, ni ngumu kumwambia achangie majengo ya shule wakati hana mtoto anayesoma eneo hilo,” anasema.

Goha anaongeza kuwa, “wananchi wanakataa kuchangia kwa madai walimu wanakula michango na ndiyo sababu ya kukosekana kwa muendelezo wa majengo katika shule hizo.”

Nyongeza (takwimu nyingine)

Loading...

Loading...