Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa: Serikali inatambua mchango wa Taasisi za dini


Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini, waamini na Watanzania kwa ujumla kuzidisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa sababu asili ya dini ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na kwa binadamu.

Tanga. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo Septemba 3, 2023 mkoani Tanga alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa askofu mpya wa jimbo la Tanga, Thomas Kiangio iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Antony wa Padua lililopo Chumbageni jijini Tanga.

Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini, waamini na Watanzania kwa ujumla kuzidisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa sababu asili ya dini ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na kwa binadamu.

“Hivyo basi, uwepo wa upendo ni msingi mzuri wa kuendelea kulinda amani tuliyonayo katika Taifa letu,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kwamba hayo yote yasingeweza kufanyika kama Taifa letu lingekuwa katika hali ya machafuko.

Ameongeza: “Hata leo tumeshiriki kwenye misa hii kwa utulivu kabisa kutokana na amani iliyopo. Sina shaka kuwa mtakubaliana nami kuwa Watanzania wote ni wacha Mungu, wanaotii sheria za Mungu na zile za Serikali na wanatambua wajibu wao wa kiroho wa kutii mamlaka zilizopo.”

Ibada ya kumweka wakfu askofu huyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeo Ruwaich aliyesema baada ya jimbo la Tanga kumkosa askofu huyo kwa zaidi ya miaka miwili, leo linampata askofu aliyechaguliwa na kristo kuwaongoza waumini.

“Kila nilipokuwa nakuja Tanga baada kifo cha Askofu Anthony Banzi, walikuwa wakiniuliza tutakaa bila askofu hadi lini? amesema Ruwaich.

Askofu huyo amesema askofu mteule hana cha kujivunia wala kujigamba bali amepatikana kutokana na huruma na upendo wa Kristo. Amesema Yesu hamkabidhi mtu yeyote utume bila ya upendo bali anapenda upendo na maelewano.

Tamko la kumkabidhi Kiangio uaskofu limesomwa na Balozi wa Papa Fransis nchini Tanzania ambapo baadaye jopo la maaskofu limeweza kumuwekea mikono ya kimsimika.

Askofu Thomas John Kiangio alizaliwa tarehe 17 Machi, 1965 katika kijiji cha Mazinde Ngua wilayani Korogwe, Tanga anakuwa askofu wa tano baada ya kifo cha aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Hayati Askofu Anthony Banzi aliyefariki tarehe Desemba 20, 2020.

Askofu Kiangio amewahi kushika nafasi za kichungaji katika Parokia ya Ekaristi Takatifu huko Lushoto na pia amehudumu katika nafasi ya Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Tanga kuanzia mwaka 2020 hadi Juni 07, 2023 alipoteuliwa kuwa Askofu Mteule. Pia, amewahi kutumikia katika nafasi ya Gombera Msaidizi (Rector).