MAHUBIRI: Nguvu iliyopo kwenye sala ya Bwana kwa Mkristo
Bwana Yesu asifiwe. Ninaitwa Neema Kisinga, karibu tena kwenye tafakari ya neno la Mungu. Somo letu leo Jumapili linatukumbusha umuhimu wa maombi katika maisha ya Mkristo.
Ninapenda kukutia moyo licha ya changamoto zote za kidunia tunazopitia bado ukiwa ndani ya Neno la Mungu upo salama.
Katika Injili ya Mathayo 6:7-13, Yesu anawafundisha wanafunzi wake namna sahihi ya kuomba. Anatuonyesha kuwa maombi siyo maonyesho mbele za watu wala kurudia maneno mengi bila kuelewa, bali ni mawasiliano ya kweli kati ya mtoto wa Mungu na Baba yake wa mbinguni.
Yesu alianza kwa kuonya dhidi ya kupayuka payuka kama watu wa mataifa. Watu hao walidhani kuwa Mungu husikia kutokana na wingi wa maneno. Lakini Yesu anafundisha kuwa Mungu wetu siyo sanamu wala Mungu asiyejua mahitaji yetu. Yeye ni Baba anayejua tunayohitaji hata kabla hatujaomba. Hivyo maombi siyo njia ya kumpa Mungu taarifa mpya, bali ni njia ya kuonyesha kwamba tunamtegemea Yeye peke yake na siyo miungu mingine.
Sala ya Bwana inaanza kwa maneno: “Baba yetu uliye mbinguni.” Haya ni maneno ya neema kubwa. Yanatuonyesha kuwa kupitia Yesu Kristo tumefanywa watoto wa Mungu. Siyo kila mtu anaweza kumwita Mungu Baba kwa maana ya wokovu, bali wale waliompokea Kristo kwa imani. Hivyo tunapoomba tunakuja mbele za Mungu si kama wageni, bali kama watoto wapendwa mbele ya Baba mwenye upendo.
Ombi la kwanza linasema: “Jina lako litukuzwe.” Hapa tunafundishwa kuwa katika maombi lazima tuanze na Mungu kwanza, siyo mahitaji yetu. Tunaliomba jina lake litukuzwe kwa mafundisho ya kweli na maisha matakatifu. Mkristo anapoitii Neno la Mungu analitukuza jina lake duniani.
Kisha tunaomba: “Ufalme wako uje.” Ufalme wa Mungu huja pale Roho Mtakatifu anapotutawala kupitia Neno lake. Tunaomba imani yetu ikue na maisha yetu yawe chini ya utawala wa Kristo. Pia tunaomba watu wengi zaidi wamjue Yesu na kuingia katika ufalme wake.
Tunapoomba: “Mapenzi yako yatimizwe,” tunajifunza kumtii Mungu. Mbinguni mapenzi ya Mungu hutimizwa bila upinzani, lakini duniani kuna dhambi na maasi. Ndiyo maana tunahitaji neema ya Mungu ili tuweze kuishi katika utii wake kila siku. Tunaomba Mungu ashinde nguvu zote za Shetani, dunia na mwili zinazotuzuia kumtii.
Katika ombi la “Utupe leo riziki yetu,” Yesu anatufundisha kuwa Mungu anajali mahitaji yetu yote ya kila siku. Chakula, afya, kazi, familia, amani na ulinzi vyote hutoka kwake. Hivyo Mkristo hapaswi kuishi kwa hofu, bali kwa kumtegemea Baba anayetoa mahitaji ya watoto wake.
Ombi la msamaha lina umuhimu mkubwa sana: “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Tunamwomba Mungu atusamehe kwa neema yake kwa sababu sote ni wenye dhambi. Pia tunafundishwa kuwasamehe wengine. Moyo usiosamehe hujifungia nje ya neema ya Mungu. Mkristo wa kweli anaishi katika toba na msamaha kila siku.
Tunapoomba: “Usitutie majaribuni,” tunaomba Mungu atulinde dhidi ya nguvu za dhambi na hila za Shetani. Dunia ina majaribu mengi yanayotaka kutuondoa kwa Mungu. Hivyo tunahitaji msaada wake kila siku ili tushinde na kubaki waaminifu.
Mwisho tunaomba: “Utuokoe na yule mwovu.” Hapa Yesu anatukumbusha kuwa Shetani ni adui wa waamini. Tunahitaji ulinzi wa Mungu dhidi ya kazi zote za uovu. Kristo ndiye mshindi wa mwisho dhidi ya Shetani, na katika yeye tunapata ushindi.
Ndugu wapendwa, maombi ni pumzi ya maisha ya Mkristo. Mkristo asiyeomba ni kama mtoto asiyesema na Baba yake. Tunapaswa kumwomba Mungu kila siku: nyumbani, kanisani, kazini, safarini na faraghani. Maombi si kazi ya ibada tu, bali ni maisha ya uhusiano na Mungu.
Mtu au Mkristo asiyeomba hupoteza uhusiano wake wa karibu na Mungu. Maombi ndiyo njia ambayo mtoto wa Mungu huwasiliana na Baba yake wa mbinguni. Anapoacha kuomba, moyo wake huanza kuwa mbali na Mungu na maisha yake ya kiroho hudhoofika.
Mara nyingi mtu asiyeomba huanza kutegemea nguvu zake mwenyewe, hekima yake au mali zake badala ya kumtegemea Mungu. Hali hii humfanya awe dhaifu mbele ya majaribu, mashaka na hofu za maisha.
Ndiyo maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake waombe ili wasiingie majaribuni. Maombi hutuweka karibu na Mungu, lakini kutokuomba hutufanya tuishi bila nguvu za kiroho.
Mkristo asiyeomba hupoteza amani na mwongozo wa Mungu. Maombi huleta faraja, matumaini na utulivu wa moyo hata katikati ya shida.
Mtu anapoacha kuomba mara nyingi moyo wake hujaa wasiwasi, kukata tamaa na mashaka. Aidha, Shetani hupata nafasi rahisi ya kumjaribu na kumpotosha. Kanisa lisiloomba hupoa kiroho, familia isiyoomba hupoteza umoja, na mtu asiyeomba hujikuta akianguka kirahisi katika dhambi. Ndiyo maana mtume Paulo 1 Wathesalonike 5:17 alisisitiza kwamba “Ombeni bila kukoma.” Maombi siyo hiari kwa Mkristo bali ni hitaji la kila siku.
Katika Biblia (1 Samweli 1:10-15) tunaona mfano wa Hana , ambaye alikuwa tasa kwa muda mrefu, alimlilia Mungu kwa uchungu mkubwa na Mungu akamsikia. Kupitia maombi yake alipokea mtoto Samweli ambaye baadaye alikuwa nabii mkuu katika Israeli.
Hii inatuonyesha kuwa Mungu husikia kilio cha watu wake hata wanapokuwa katika hali ngumu kiasi gani. Hana hakukata tamaa bali alimwendea Mungu kwa imani na akapata jibu.
Pia tunamwona Nehemia 1:1-11, Nehemia alipoombea taifa la Israeli na kuomba rehema ya Mungu kuhusu Yerusalemu iliyokuwa imeharibika. Mungu alimfungulia njia mbele ya mfalme na akafanikiwa kuijenga upya kuta za Yerusalemu. Mafanikio yake hayakutokana na nguvu zake binafsi bali kutokana na maisha ya maombi. Nehemia alijua kuwa ushindi wa kweli huanza kwa kupiga magoti mbele za Mungu kabla ya kuanza kazi yoyote.
Matendo ya Mitume tunasoma kuwa kanisa la kwanza lilidumu katika maombi. Walipokutana na mateso walimwomba Mungu na wakajazwa ujasiri pamoja na nguvu za Roho Mtakatifu. Petro alipowekwa gerezani, kanisa lilikesha katika maombi na Mungu akamtuma malaika kumfungua. Hivyo Biblia inathibitisha wazi kuwa watu wanaomtegemea Mungu kwa maombi hupokea msaada, ushindi na nguvu mpya katika maisha yao
Tumuendee Baba yetu kwa imani, tukijua kuwa anatupenda, anatuhitaji tukae karibu naye, na anatusikia. Mungu atujalie maisha ya maombi siku zote. Amina.
Neema Kisinga ni anapatika Iringa, kwa ushauri na maombi 0714840100.