Prime
Mahakama yapokea video kesi ya ubunge wa Baba Levo, yakataa barua ya onyo kwa CCM
Muktasari:
- Mbunge wa Kigoma Mjini, maarufu kwa jina la Baba Levo, anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.
Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imepokea diski mweko (flash disk) mbili zenye picha jongefu (video) zaidi ya 45 na kuziweka kuwa vielelezo vya ushahidi katika kesi ya ubunge wa Kigoma Mjini inayomkabili Mbunge wa jimbo hilo, Clayton Chipando (CCM).
Hata hivyo, Mahakama hiyo imekataa kupokea nakala kivuli ya barua ya onyo kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini, ikisema haijakidhi matakwa ya kisheria.
Mahakama imepokea vielelezo hivyo kupitia shahidi wa 16 katika kesi hiyo, Abdul Nondo, wakati akitoa ushahidi wake mahakamani hapo leo, Julai 10, 2026.
Shahidi huyo, kabla ya kuanza kuhojiwa maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake wa maandishi, ameiomba Mahakama ipokee flash disk yenye picha jongefu (video) zaidi ya 40 na kuomba video hizo zionyeshwe mahakamani.
Hata hivyo, maombi hayo yalipingwa na mawakili wa walalamikiwa.
Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, amedai kuwa hawapingi kupokelewa kwa flash disk hiyo mahakamani, bali wanapinga maombi ya video zilizomo kuoneshwa, akidai kuwa maombi hayo hayakuandikwa wala kuombwa katika ushahidi wake wa maandishi.
Kwa upande wa wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, pia amepinga pamoja na mambo mengine akidai kuwa shahidi hajaweka msingi wa kupokelewa kwa flash disk hiyo.
Akijibu hoja hizo, wakili wa walalamikaji, John Seka, amedai kuwa shahidi huyo ameweka msingi wa kupokelewa kwa flash disk hiyo kuwa kielelezo cha ushahidi wake.
Akitoa uamuzi, Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo amekubaliana na maombi ya shahidi Nondo na kuipokea flash disk hiyo pamoja na maudhui yaliyomo.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 19 cha Sheria ya Ushahidi wa Kielektroniki, shahidi huyo ameeleza maudhui hayo katika maelezo yake.
"Hivyo, Mahakama hii inaipokea flash disk hii pamoja na yote yaliyomo na kuwa kielelezo cha ushahidi wa shahidi huyo," amesema Jaji Nongwa.
Kuhusu kuonyeshwa video hizo, Jaji Nongwa amesema kuwa kutokana na muda, haitawezekana kuonyeshwa zote, lakini akaelekeza kuwa kama mawakili wa walalamikaji wakati wa maswali ya dodoso watahitaji kuangalia jambo fulani, watafanya hivyo kwa jambo husika.
Pia, shahidi huyo ameiomba Mahakama ikakubali kupokea flash disk nyingine kuwa kielelezo cha ushahidi wake. Upande wa walalamikiwa haukuwa na pingamizi na Mahakama ikaipokea kuwa kielelezo kingine cha ushahidi wake.
Vilevile, Nondo ameiomba Mahakama hiyo kupokea barua ya onyo kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, David Uwezo, kwenda kwa Chama Cha Mapinduzi, kuwa kielelezo cha ushahidi wake.
Wakili Method amepinga kupokelewa kwa barua hiyo kwa madai kuwa ni nakala kivuli na shahidi hajaweka msingi wa kwa nini awasilishe nakala hiyo, pia hajatoa ushahidi kama aliomba nakala halisi kwa mujibu wa Kifungu cha 74 cha Sheria ya Ushahidi.
Pia, Wakili Method alidai kuwa nyuma ya barua hiyo kuna mambo mengine ambayo shahidi hajayazungumzia, hoja ambayo iliungwa mkono na wakili wa Baba Levo, Msasa.
Hata hivyo, Wakili Seka amedai kuwa shahidi huyo ameweka msingi katika maelezo ya ushahidi wake wa maandishi ambapo ameeleza kuwa alichoweza kupata ni nakala kivuli.
Amedai kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 73 cha Sheria ya Ushahidi, nakala kivuli inaweza kupokelewa kama nakala halisi haiko katika miliki ya mwombaji.
Pia, amedai kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(e) cha sheria hiyo, nakala kivuli inaweza kupokelewa kama nyaraka hiyo inayorejelewa iko kwenye umma.
Wakili Seka amedai kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 74 kilichotumiwa na wakili wa Serikali, kinataka kutolewa notisi, lakini akasema kuna mazingira ambayo sharti hilo la notisi halihitajiki na kwamba nyaraka hiyo inaangukia katika mazingira hayo.
Vilevile, Wakili Seka amedai kuwa wanaamini nakala halisi ipo kwa mlalamikiwa wa kwanza (Msimamizi wa Uchaguzi), kwani ndiye mmiliki wa barua hiyo halisi.
Hata hivyo, Wakili Vivian amesema kuwa ili mtu anufaike na Kifungu cha 73 ni lazima awe amekidhi matakwa ya Kifungu cha 74, ambacho kinataka kutolewa kwanza notisi ya kuwasilisha kielelezo hicho ambacho si halisi.
Vilevile amesema nakala halisi ya barua hiyo haiko katika mahakama hii (kwa mlalamikiwa wa kwanza), na kwamba iliyopo ikilinganishwa na nakala kivuli inayoombwa kupokelewa kuna tofauti katika mambo mengi.
Wakili Msasa pia kwa upande wake amesisitiza kuwa bado wanapinga kupokewa kwa barua hiyo, kwani ina viambatanisho ambavyo wao hawajawahi kupewa.
Hata hivyo, Jaji Nongwa katika uamuzi wake amesema kuwa ni wazi hakuna notisi iliyotolewa na hivyo mahakama haiwezi kuipokea barua hiyo ambayo ni nakala kivuli.
"Hivyo mahakama hii haiwezi kuipokea nakala ya barua hiyo kwa kuwa haijakidhi matakwa ya sheria," amesema.
Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo ameendelea na ushahidi wake katika hatua ya maswali ya dodoso.
Kesi yenyewe
Baba Levo alitangazwa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne wanaojitambulisha kama wapigakura wa Jimbo la Kigoma Mjini, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu, wamefungua kesi kupinga ushindi wake.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, vikiwemo vitendo vya rushwa na udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba Mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura, kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.