Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuriko yanavyowatesa wakazi wa mitaa minne Dodoma

Muktasari:

  • Kwa miaka minne mfululizo, wakazi wa mitaa minne ya Kata ya Nkhungu, Wilaya ya Dodoma Mjini, wamekuwa wakikumbwa na adha ya mafuriko kila mvua zinapoanza kunyesha.

Dodoma. Upo msemo wa Kiswahili usemao, "kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake," unaomaanisha kuwa changamoto za mtu hufahamika vyema zaidi na yule anayezipitia.

Msemo huu unathibitishwa na wakazi wa mitaa ya Bochela, Mtube, Mnyakongo, na Salama, Kata ya Nkhungu, Dodoma, ambao kwa miaka minne mfululizo wanalazimika kuhama makazi yao kwa miezi isiyopungua minne kutokana na mafuriko.

Changamoto kubwa inayowakumba wakazi wa eneo hilo ni uwepo wa bwawa la maji katikati ya makazi yao, ambalo limekuwa chanzo cha mafuriko na hatari kwa watoto. Bwawa hilo pia limekuwa likisababisha vifo vya watoto wanaovua samaki kwenye visima vilivyochimbwa pembeni kwa shughuli za umwagiliaji.

Licha ya jitihada za kuweka uzio wa seng’enge kuzunguka Shule ya Msingi Mnyakongo iliyoko karibu na bwawa hilo, watoto bado wanatoroka na kwenda kuvua samaki.

Tukio la hivi karibuni lilisababisha kifo cha mwanafunzi wa shule hiyo aliyejulikana kwa jina la Playgod, aliyefariki Novemba 2024.

Mwalimu wa darasa la kwanza katika shule hiyo, Modesta Phabian, amesema kuwa huyo ni mtoto wa pili kufariki katika bwawa hilo tangu shule hiyo ianzishwe miaka mitatu iliyopita.


Historia ya Mafuriko

Akizungumza na Mwananchi, leo Januari 21, 2025, Augusta Clemence, mkazi wa Mtaa wa Mnyakongo, anasema mafuriko yalianza mwaka 2019/2020 baada ya mvua kubwa kunyesha. Tangu wakati huo, nyumba zimekuwa zikipata athari kubwa, huku wakazi wakilazimika kuhama mara kwa mara.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kuondoa maji haya kwa kuyatembeza badala ya kukaa mahali pamoja kama sahani. Tukisaidiwa, tutaweza kuendeleza nyumba zetu,” anasema Augusta.

Naye Jane Justine, mkazi wa Mbwanga Bwawani, anasema alijenga nyumba katika eneo hilo kwa nia ya kuepuka gharama za kupanga, lakini mafuriko yamelazimu kuhama mara kwa mara.

Jane anaeleza kuwa walijiunga na wanawake wengine kuomba Serikali kuchimba mitaro ya kuondosha maji, jambo lililosaidia kupunguza tatizo kwa kiasi fulani, lakini maji kutoka kwenye mabwawa mengine bado yanajikusanya katika bwawa hilo.


Vifo na hofu kwa wakazi

Ana Peter, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, anasema hali ni hatari zaidi watoto wanapoingia bwawani kucheza au kuvua samaki.

“Tunaiomba Serikali itoe hili bwawa kwa sababu wananchi wengi wameathirika. Ukija ukiangalia shule ipo karibu halafu watoto wanatoka kule (shuleni), wanakuja wanaingia hapa (bwawani) wanachezea haya maji ambayo ni mabaya kwao,”anasema.

Agnes Mgumba, mkazi mwingine, anaungana na wenzake kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuwa hali ya kuhama mara kwa mara imekuwa changamoto kubwa kwa familia nyingi.


Serikali yachukua hatua

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnyakongo, Hector Stephano, anasema Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kuondosha maji kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Mradi huo ni sehemu ya Mpango wa Kuboresha Miji 45 (TACTIC) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambao ulianza Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Februari 19, 2025.

Mratibu wa Mradi wa TACTIC, upande wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nicodemus, anasema kuwa miradi inahusisha kuchimba mifereji na mabomba ya kuondosha maji kuelekea Hombolo, kupitia Kisima cha Nyoka. Mradi huo, ambao utagharimu Sh24.093 bilioni, unalenga kutatua tatizo la mafuriko na kuboresha maisha ya wakazi wa Kata ya Nkhungu.


Mwito kwa serikali

Wakazi wa mitaa hiyo wanaiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyopo ili kuwapa ahueni na kuepusha vifo vinavyotokana na mafuriko.

Mwenyekiti wa mtaa, Stephano, anashauri ufuatiliaji wa karibu kwa wakandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.