Mafuriko Arusha yaahirisha maandamano Chadema

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini,Amani Golugwa.

Muktasari:

  • Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema maandamano hayo yalipangwa kufanyika wilayani Karatu, Aprili 25, 2024 sasa yameahirishwa hadi watakapotangaza maandamano ya awamu ya pili.

Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesogeza mbele maandamano ya amani yaliyopangwa  kufanyika mkoani Arusha Alhamisi ya Aprili 25, 2024, kufuatia Wilaya ya Karatu walipopanga kuyafanya kukumbwa na mafuriko.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2024 na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa  akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo. Maandamano hayo yalipangwa kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu.

"Tulipanga maandamano yafanyike Karatu ila kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, wilaya ile imekumbwa na mafuriko yaliyosababisha  makazi ya watu ikiwemo wanachama wetu kuzingirwa na maji.

"Hivyo tumeona siyo busara kufanya maandamano kukiwa na hali ile, tunafanya mchakato wa kuhakikisha tunawapatia msaada wa kibinadamu na tunaahirisha maandamano  hadi awamu ya pili.

“Kwa sasa yatafanyika katika majimbo ya Babati Mjini (Manyara), Moshi Mjini na Tanga Mjini ,"amesema Golugwa.

Akizungumzia uchaguzi wa Kanda, Golugwa amesema wanatarajia kuanza na chaguzi ngazi za vitongoji na ndani ya miezi miwili watakuwa wamemaliza na wataanza  wa Kanda.

"Kwa sasa tunaanza na chaguzi za ngazi za chini kabisa na tunatarajia uchaguzi wa Kanda hasa ikizingatiwa hii ni ngome ya chama, tutaona joto la uchaguzi lakini pia utafanyika kwa ustaarabu wa aina yake,” amesema Golugwa.