Maelekezo matano ya Waziri Mkuu kuimarisha uwekezaji Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Taarifa za Maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara pamoja na Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji, Ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es salaam. kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kulia Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo. Picha na owm_tz.
Muktasari:
- Septemba 11, 2024 kumezinduliwa taarifa za maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara na Nyenzo za usimamizi wa uwekezaji nchini Tanzania iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameelekeza taasisi pamoja na mamlaka za serikali za mitaa ziharakishe marekebisho ya taratibu na sheria zinazochangia urahisi wa kufanya biashara.
Amesema zihakikishe sheria mpya zinawezesha mazingira bora ya biashara na uwekezaji kila eneo huku likienda sambamba na kuweka kipaumbele katika kutoa huduma kwa haraka.
"Mamlaka ziwe na mifumo rahisi ya kuwasilina kwa wawekezaji na wafanyabiashara wetu kwenye maeneo yao na kuondoa vikwazo vinavyokwaza uwekezaji kwenye eneo husika," amesema.
Ametoa maelekezo hayo jana usiku Jumatano ya Septemba 11, 2024 kwenye hafla ya uzinduzi wa taarifa za maboresho ya Mazingira ya Uwekezaji na Biashara na Nyenzo za usimamizi wa uwekezaji nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Pili, amesema taasisi na mamlaka hizo ziongeze ushirikiano wa karibu na sekta binafsi kwani zinaweza kutoa mawazo na mapendekezo yenye thamani kuhusu maboresho yanayohitajika.
"Aidha, wekeni mipango ya kutoa mafunzo na huduma kwa wadau wa biashara ikiwa pamoja na uhamasishaji wa matumizi wa nyenzo mpya za usimamizi na uwekezaji. Kuhakikisha jamii pia inashirikishwa katika michakato ya uboreshwaji ili kupokea maoni yao na kuhakikisha maamuzi yanayochukuliwa yanawiana na mahitaji ya jamii husika," amesema.
Tatu, amesema taasisi zote zinazoshughulikia uwekezaji na biashara zinapaswa kuwekeza kwenye mifumo ya Kieletroniki ya habari na mawasiliano ili kuboresha usimamizi na kuondoa urasimu. Lakini muhimu ni kuongeza uwazi katika kuendesha mifumo.
Nne, taasisi zetu za Serikali tuweke mifumo ya tathmini ya mara kwa mara na mikutano kati ya wafanyabiashara na wawekezaji kuwapa nafasi kueleza changamoto zao kushirikiana katika kutatua sambamba na kutathimini maboresho katika kipindi kilichopita.
Amesema mwisho taasisi zetu hasa za ukaguzi wa bidhaa maeneo ya kupokelea bidhaa hizo zikae kwa pamoja ziwe zinakagua kwa pamoja akitaja ikiwemo Osha, Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Zimamoto kwa lengo la kupunguza kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji wetu nchini.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuendelea kufanya maboresho ya uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa kinara katika sekta hiyo.
Akitolea mfano amesema halmashauri 184 kuna idara za viwanda na uwekezaji ambapo huduma zote zinapatakina katika ngazi ya halmashauri pamoja na mkoani.
Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya Tehama ikiwemo kusomana kwa taasisi za Serikali ili kuwezesha wawekezaji kujisajili ikiwemo kupata vibali vya uwekesaji ndani ya muda mfupi.
"Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuwaunga mkono katika shughuli zenu za biashara na uwekezaji na amesema atahakikisha mnapata manufaa na tija," ametuma salamu hizo.
Katika hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu wake Dk Doto Biteko, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na viongozi wengine wa Chama na Serikali.
Taarifa ya kwanza aliyozindua Waziri Mkuu ni taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na wafanyabiashara nchini. Taarifa ya pili inahusu muongozo wa uendelezaji wa usimamizi wa maeneo maalumu ya kiuchumi.
Pia, Ripoti ya taifa ya uwekezaji ya mwaka 2023. Mpango mkakati wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa mwaka 2024/25 hadi 2025/26. Mfumo wa kieletroniki wa kuwahudumia wawekezaji wote nchini kwenye programu ya maeneo maalumu ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja ofisi yake imeandaa rasimu ya sera mpya ya uwekezaji ya mwaka 2024 itakayochukua nafasi ya sera ya mwaka 1996.
Amesema tathmini iliyofanyika kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara (Mkumbi) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ambao unaonesha unafanya vizuri.
Ilichokisema TPSF
Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Raphael Maganga yeye amepongeza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini (Mkumbi).
Amesema TPSF imeona jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuondolewa kwa tozo mbalimbali, zaidi ya sheria 55 kufanyiwa marekebiesho pamoja na mifumo ya kieletroniki zaidi ya 119 kuendelea kusomana.
"TPSF tunashauri Serikali kuwa na sera zisizobadilika badilika vilevile kurudisha imani katika sekta ya mabenki baada ya wafanyabiashara kufungiwa akaunti na fedha zao kuchukuliwa hapo nyuma ili waendelee na moyo wa kuendelea na biashara zao," ameshauri Maganga.
Chalamila alilia Sera, Sheria zisizobadilika kuinua uchumi wa buluu, uwekezaji
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema lazima kama taifa tuwe na Sheria na Sera nzuri zisizobadilika badilika ili kuvutia wawekezaji.
Amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam ni wadau wakubwa wa Uchumi wa Buluu huku akibainisha bado hawafanyi vizuri katika sekta hiyo kwakuwa hakuna sheria wala sera nzuri.
"Mfano, ukiangalia kwenye masuala ya usafirishaji wa majini sera yake ni pana sana kiasi kwamba, Wadau wa Dar es Salaam tunatamani Waziri mwenye dhamana aendelee kuichimba sera hiyo iwe maalumu kwenye masuala ya usafirishaji majini na uchumi wa buluu," amesema Chalamila.
Hata katika uvuvi wa bahari kuu amesema: "Uvuvi wa bahari kuu sera yake bado haijawa nzuri kwa mantiki hiyo ili tuweze kuzama na kuweka mazingira mazuri ni vizuri tujikite huko ili mambo yazidi kuwa mazuri."
Ameongeza hata bandarini kuna sera iitwayo ‘Nne kwa Mbili’ ikiwa na maana makontena yanayokuja na mizigo kutoka nchi mbalimbali duniani yale makasha yanatakiwa kurudi yalipotoka yakiwa tupu kwa angalau asilimia 50.
"Makasha yanapaswa kurudi tupu hivyo ni ushahidi hatuna mizingo mingi ya kupeleka nje. Tunatakiwa kubalance uingizaji na upelekaji nje wa mizigo ya bidhaa zetu za Kitanzania, ili makasha yanayokwenda nje yaende na bidhaa zetu," amesema.