Mabilioni yamwagwa ujenzi Uwanja wa Ndege Musoma

Muktasari:
- Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Sh35 bilioni kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma mkoani Mara.
Musoma. Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Sh35 bilioni kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma mkoani Mara.
ujenzi huo utahusisha njia ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa kilomita 1.6, maegesho ya ndege, jengo la zima moto na vifaa vya kuoNgozea ndege.
Akitoa taarifa leo Ijumaa Aprili 16, 2021 kwa naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara aliyeko mkoani Mara, meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Felix Ngaile amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo amepatikana na wiki mbili kuanzia leo ataanza kazi.
Amebainisha kuwa mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya China Beijing Construction itatekeleza mradi huo kwa miezi 20.
Amesema uwanja huo utajengwa kwa awamu tatu, ya pili itahusisha ujenzi wa jengo la abiria huku awamu ya tatu ikihusisha uwekaji taa.
Ngaile amesema hadi sasa haijajulikana awamu ya pili na tatu zitagharimu kiasi gani cha fedha, “awamu ya kwanza ikikamilika kwenye uwanja huo ndege za ATR 42 na ndege nyingine zitaweza kutua. Ndege ya Q400 itaweza kutua ila kwa maelekezo maalum.”
Meneja wa uwanja huo, Mohamed Makao amebainisha kuwa ndege zenye ratiba maalum zilizitisha safari zake katika uwanja huo mwaka 2018 baada ya miundombinu ya uwanja kutokuwa rafiki.
Amefafanua kuwa hivi sasa ndege zinazotua na kuruka katika uwanja huo ni binafsi na kukodi huku asilimia 98 ya abiria wa uwanja huo ni wale wanaotoka nje ya nchi na asilimia mbili ni wa ndani.
“Abiria wanaotua katika uwanja imeshuka kutoka abiria 7,931 mwaka 2018 hadi abiria1,020 mwaka 2020. Miruko ya ndege imeshuka kutoka 932 mwaka 2018 hadi 427 mwaka 2020, sababu ni ugonjwa wa corona na miundombinu mibovu,” amesema.
Naye Waitara amesema kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia kuchochea uchumi wa mkoa na Taifa kutokana na fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Mara ikiwemo utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti..
Amebainisha kuwa ujenzi huo utakuwa wa kihistoria kwani uwanja huo tangu ujengwe wakati wa uongozi wa rais wa awamu ya kwanza, Hayati Julius Nyerere haujawahi kuwekewa lami.