Latra yajipanga nauli treni za SGR Dar - Dom

Wajumbe wa Bodi ya Wakugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra), wakitembelea kukagua Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam, Dodoma inayotarajia kuanza kutoa huduma Julai mwaka huu.
Muktasari:
Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) inakamilisha, upangaji wa viwango vya nauli za treni za mwendo wa haraka, vitakavyotumika baada ya huduma kuanza rasmi kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) inakamilisha, upangaji wa viwango vya nauli ya treni za mwendo wa haraka vitakavyotumika baada ya huduma kuanza rasmi kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Shirika la Reli Tanzania TRC lilipendekeza viwango mbalimbali vya nauli za abiria kwa treni ya SGR, huku Latra ikiitisha maoni ya wadau ikiwa ni utekelezaji wa kifungu Na 21 cha Sheria Na 3 ya Latra ya mwaka 2019.
Agizo la kuanza kutoa huduma ya treni hizo ifikapo Juni mwaka huu, lilitolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Desemba 2023 wakati akitoa salamu za mwaka mpya.
Akizungumza Ijumaa Februari 2, 2024 baada ya bodi ya wakurugenzi ya Latra kutembelea mradi wa SGR, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema, mambo mengi ya kiufundi yamekamilika na sasa wapo katika majaribio yanayotakiwa kufanyika kabla ya kutoa huduma ili kulinda usalama.
“Mfumo umeshajengwa mtu atatakiwa kuingia na kadi yake au kwa kutumia karatasi itakayokuwa imetoka kwenye mashine, hivyo tanakwenda kukamilisha upangaji wa nauli ili ifikapo Julai tuwe tumekamilisha,” amesema Suluo.
Amesema walianza mchakato wa kupanga nauli za SGR, wakati huo mabehewa yalikuwa hayajaja ndipo walipotoa maelekezo kwa TRC baada ya kuyakagua na kuona ubora wake kwa kila daraja
“Kutakuwa na madaraja tofauti yakiwemo ya biashara na ya kawaida, hivyo nauli ni lazima zitofautiane. Baada ya kuwasili mabehewa tuliona tuangalie pale tulipoishia, TRC watuletee gharama za uwekezaji ili wasirudi serikalini kuomba uendeshwaji wa hii SGR,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Senzige Kisenge alisema yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyika kabla ya kuanza kutoa huduma ili kulinda usalama, hivyo ni lazima kufanya majaribio.
Amesema majaribio wanayofanya ni njia yenyewe pamoja na kichwa, kulingana na mpango waliojiwekea kwa msaada wa msimamizi.
Awali Mwenyekiti bodi ya Latra, Profesa Ahmed Mohamed Ame amesema ziara hiyo ni kutaka kufahamu walipofikia hasa mambo ya kitaalamu na kisheria ili ifikapo Julai waweze kuanza kutoa huduma.