LAAC yashtukia ‘upigaji’ ujenzi wa hospitali kwa Sh1.8 bilioni
Mwenyekiti wa Timu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Halima Mdee (kushoto) akiongea katika kikao cha majumuisho baada ya kufanya ziara ya siku tatu mkoani Mtwara akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas (kulia). Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema kuwa ina mashaka juu ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Mji Nanyamba Sh1.8 bilioni zilitolewa na serikali zilivyotumika katika ujenzi wa hospitali huku waliohusika wakiwa hawajachukuliwa hatua yoyote.
Mtwara. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema kuwa ina mashaka juu ya masuala ya ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa hospitali ya Mji Nanyamba namna ulivyoshughulikiwa.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho leo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Halima Mdee alisema kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2018 na kutengewa fedha zaidi ya Sh1.8 bilioni.
“Kwa kweli kamati ina mashaka juu ya masuala ya ubadhirifu yaliyvyoshughulikiwa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Nanyamba namna Sh1.8 bilioni zilitolewa na serikali zilivyotumika katika ujenzi wa hospitali hiyo,” amesema.
“Tumeambiwa suala hili liko mikononi mwa Takukuru liko huko kwa zaidi ya miaka miwili ni vyema ukafuatiliwa na mchakato utaolewa na mkuu wa wilaya hii naamini atatusaidia kupata suluhu kwa hili,” amesema.
“Katika ujenzi huo upo ubadhirifu ulifanyika ikiwemo milango hewa 87, mabati ya shiligi milioni 9, vitasa na saruji ambapo haujachukuliwa hatua kikamilifu kwa nia ya kuukomesha kwani hakuna hatua zilizochukuliwa miongoni mwa wahusika,” amesema.
Katika hatua nyingine kamati imeitaka ofisi ya Tamisemi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kiasi cha shilingi milioni 106 ili kuipata tofauti ya shilingi milioni 19 kisha kuchukua hatua kali kwa watumishi waliochota fedha kwa manufaa yao,” amesema.
“Masasi, Nanyamba na Mtwara walitoa mikopo ya shilingi bilioni 3.1 na kurejesha shilingi bilioni 2.2 huku shilingi milioni 900 zikibaki kwa wakopaji. Mwenendo huu unakupa picha ya kuona tatizo hili lina ukubwa kiasi gani,” alihoji Mdee.
Kwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Dk Wilson Charles alisema kuwa ni vyema watumishi wakatambua kuwa wanatakiwa kushirikiana na Serikali ili kuboresha maisha ya Watanzania ili tuweze kuingia katika uchumi wa kati.
“Watumishi acheni kutanguliza maslahi yenu kwanza tangulizeni ya Taifa na taasisi kuna ule utaratibu wa fedha zikiletwa mnabuni mbinu za kuchukua, uishe na ukomeshwe kwa atakayedhubutu ataumia, Nasisitiza tuwe waadilifu hasa fedha zikiletwa na serikali zisimamiwe vizuri na mjipange kuzisimamia vizuri,” alisema alisema Dk Charles.